De Bruyne kwenye mjadala wa Gerrard, Lampard na Scholes

Muktasari:
- Supastaa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ataachana na Man City baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muongo mmoja wa kubeba mataji tofauti na kuwa mchezaji muhimu kikosini.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO fundi wa boli, Kevin De Bruyne ataachana na Manchester City mwishoni mwa msimu huu wa 2024-25, wakati mkataba wake utakapofika ukomo huko Etihad.
Supastaa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji ataachana na Man City baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muongo mmoja wa kubeba mataji tofauti na kuwa mchezaji muhimu kikosini.
Kocha Pep Guardiola hakuwa na chakufanya zaidi ya kumwaga tu machozi wakati mchezaji huyo alipokuwa akiaga itakapofika mwisho wa msimu huu atakusanya virago vyake na kwenda kutafuta maisha kwingineko.
De Bruyne anaondoka kwenye kikosi cha Man City huku akiacha rekodi tamu kabisa za Ligi Kuu England zinazomfanya ashindanishwe na magwiji wa ligi hiyo waliwahi kutamba kwenye timu vigogo kama Chelsea, Liverpool na Manchester United.
De Bruyne aliwasili Man City akitokea Wolfsburg ya Ujerumani mwaka 2015 akiwa na mengi ya kuthibitisha kwenye kikosi hicho cha Etihad baada ya kufunguliwa mlango wa kutokea huko Chelsea.
Na baada ya kutua Man City, De Bruyne alikwenda kupata mafanikio yasiyoelezeka na kujiweka kwenye kundi bora kabisa la wanasoka waliowahi kukipiga kwenye Ligi Kuu England – na kuingia kwenye mjadala wa kuwa kiungo mchezeshaji bora aliyepata kutokea kwenye ligi hiyo.
Akiwa kinara kwenye zama za Pep Guardiola, De Bruyne amekiongoza kikosi hicho kufanya vizuri na kuwa mtu muhimu kwenye mafanikio ya timu hiyo, ikibeba mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England, Klabu Bingwa Dunia na makombe mengine ya michuano ya ndani.
Ubora wake umemfanya De Bruyne kuingia kwenye orodha ya viungo matata kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England, sambamba na Frank Lampard, Steven Gerrard na Paul Scholes.
Baada ya tangazo lake la kwamba ataondoka Man City mwishoni mwa msimu huu, jambo hilo limeibua mjadala mkubwa huko England na mashabiki wanabishana Mbelgiji anapaswa kuwekwa kwenye namba ngapi mbele ya wakali hao, Gerrard, Lampard na Scholes.
Mjadala huo unahusisha mambo mbalimbali ikiwamo takwimu, viwango na mataji, yamewekwa kwenye uchambuzi wa pamoja wa kuhusu wachezaji hao ili kuona ni nani anapaswa kuwa wapi katika kuonyesha viungo wote hao hawakuwa watu wa kawaida kwa zama zao walizokuwapo katika soka la Ligi Kuu England.
Takwimu hizo zinahusu mikikimikiki ya Ligi Kuu England pekee bila ya kuhusisha michuano mingine ambayo walizitumikia timu zao.
KEVIN DE BRUYNE – MAN CITY
Huduma ya De Bruyne kwenye kikosi cha Man City haijawahi kuwa na shaka kwa kipindi chote alichotumikia timu hiyo, akitumika kama silaha muhimu kabisa ya kocha Guardiola katika kufikia mafanikio yake ndani ya miamba hiyo ya Etihad. De Bruyne anaondoka huku akimwachia Guardiola mzigo mkubwa wa kutafuta mchezaji wa kuziba pengo lake huko Etihad, kitu ambacho kinaonekana kigumu.
Mechi: 287
Ameanzishwa: 246
Kutokea benchini: 41
Mataji ya ligi: 6
Mabao: 72
Asisti: 121
Mabao ya penalti: 4
FRANK LAMPARD - CHELSEA
Kwenye kikosi cha Chelsea, Lampard amekuwa na rekodi matata kabisa ikiwamo kuwa kinara wa mabao wa klabu hiyo yenye maskani yake Stamford Bridge. Kinachovutia kuhusu kiungo huyo wa zamani wa England, kwamba yeye ndiye anayeongoza kwa mabao The Blues. Lampard anabaki kuwa mtu kwenye heshima kubwa kwenye kikosi cha The Blues, akiwahi kupewa pia mikoba ya kuinoa timu hiyo.
Mechi: 611
Ameanzishwa: 546
Ametokea benchini: 65
Mataji ya ligi: 3
Mabao: 177
Asisti: 118
Mabao ya penalti: 43
STEVEN GERRARD – LIVERPOOL
Mr Liverpool ndivyo mashabiki walivyokuwa wakimfahamu kiungo Gerrard kutokana na mavitu yake aliyokuwa akionyesha uwanjani anapokuwa ndani ya uzi wa miamba hiyo ya Anfield. Soka lake lilimfanya aingizwe kwenye mjadala wa muda mrefu wa kuhusu nani kiungo mahiri kati yake na wawili Lampard na Scholes, kabla ya sasa De Bruyne naye kuingizwa kwenye mjadala huo wa ubora.
Mechi: 504
Ameanzishwa: 466
Kutokea benchini: 38
Mataji ya ligi: 0
Mabao: 121
Asisti: 97
Mabao ya penalti: 32
PAUL SCHOLES – MAN UNITED
Zinedine Zidane aliwahi kukiri kwamba kama kuna mchezaji aliyekuwa akimpa wakati mgumu ndani ya uwanja kwenye mechi basi ni kiungo Paul Scholes. Staa huyo wa zamani wa Manchester United alikuwa na ufundi mkubwa ndani ya uwanja, akiwa na uwezo wa kupiga pasi za aina zote ndefu na fupi, huku viungo mahiri kama Andres Iniesta na Xavi wote wakimwona Scholes kama shujaa wao.
Mechi: 499
Ameazishwa: 404
Ametokea benchini: 95
Mataji ya ligi: 11
Mabao: 107
Asisti: 82
Mabao ya penalti: 1