Cetics, Dallas kucheza fainali NBA?

Muktasari:
- Tatum ambaye aliiongoza Celtics kutwaa ubingwa wa rekodi ya NBA kwa timu moja kufikisha mataji 18 ambayo ni mengi zaidi ikiiacha Los Angeles Lakers ya LeBron James na makombe 17.
ITAJIRUDIA KWELI? Kauli ya supastaa namba moja wa mabingwa watetezi wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), Jayson Tatum wa Boston Celtics kwamba fainali ya msimu uliopita itaikutanisha timu yao dhidi ya Dallas Mavericks msimu ujao imeshtua wengi waliobaki kusubiri kama itatokea.
Tatum ambaye aliiongoza Celtics kutwaa ubingwa wa rekodi ya NBA kwa timu moja kufikisha mataji 18 ambayo ni mengi zaidi ikiiacha Los Angeles Lakers ya LeBron James na makombe 17.
Tatum ambaye pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Marekani kilichotwaa ubingwa wa Olimpiki nchini Ufaransa mwaka huu, ameacha mjadala ambao hauna majibu zaidi ya kusubiri hatua ya mtoano msimu ujao na hatimaye timu bingwa kila ukanda kama itajirudia kwa Celtics na Dallas. Hapa ndipo unapata nafasi ya kuzitazama timu zenye nafasi kubwa ya kuzizuia hizo mbili.
MINNESOTA TIMBERWOLVES
Hadi kuelekea mwezi mmoja wa mwisho kuanza kwa ligi ndefu (regular season), timu yenye odds za kucheza fainali msimu ujao ukiachana na Celtics ni Minnesota Timberwolves ya ukanda wa Magharibi ambayo ilipewa nafasi kubwa ya kucheza hatua hiyo, lakini ikashindwa kumaliza mbele ya Dallas Mavericks. Timberwolves inayoongozwa na Anthony Edwards anayepewa nguvu na Karl-Anthony Towns na Rudy Gobert, inapewa nafasi kubwa ya kurudia ubora wa msimu jana kucheza fainali dhidi ya bingwa yeyote wa Mashariki.
DENVER NUGGETS
Ukiachana na Timberwolves wanaopewa nafasi kubwa ya kucheza fainali na kuzuia fainali isijirudie, timu inayofuatia kwa kupewa nafasi kubwa ya kucheza fainali ni Nuggets waliopo Magharibi ambao wametoka kucheza fainali 2023 walipobeba taji mbele ya Miami Heat ya Mashariki.
Ili kufika fainali mwaka jana, Nuggets waliwatoa nishai Lakers kwa ufagio (sweep) wa mechi nne na msimu uliopita pia wakaiondosha timu hiyo kwenye robo fainali kabla ya kwenda kutolewa na Timberwolves kwenye nusu fainali.
MVP Nikola Jokic ndiye kinara wa Nuggets ambaye akiwa fiti ni tatizo kwa timu pinzani kiasi cha kuifanya iwe na matarajio makubwa ya kucheza fainali kama atakuwa fiti pamoja na nguvu ya uwepo wa nyota wawili Jamal Murray na Russell Westbrook aliyeongezwa.
NEW YORK KNICKS
Kutoka Mashariki, Knicks ndiyo timu inayopewa nafasi kubwa ya kuzuia Celtics isirudi kwenye fainali msimu ujao kutokana ubora wa kikosi kikiongozwa na Jalen Brunson, Donte DiVicenzo, Julius Randle, OG Anunoby na staa mpya Mikal Bridges. Timu nyingine kutoka upande huo inayoweza kuizuia Celtics isirudi fainali ni Milwaukee Bucks ya Giannis Antetokoumpo na Damian Lillard.
PHOENIX SUNS
Msimu uliopita Suns ilipewa nafasi ya kucheza fainali ukanda wa Magharibi, lakini kutokana na ukanda huo kutoeleweka mara zote hadi fainali ifike, msimu huu pia siyo ya kuiweka pembeni kucheza fainali ili kuizuia Dallas kutorudia fainali dhidi ya Celtics kama itafanikiwa upande wa Mashariki. Bado Suns iliyocheza fainali NBA 2021, ina nafasi ya kurudia kutokana na kuwa na utatu mkali na tishio wa Kevin Durant, Devin Booker na Bradley Beal ambao kama watakuwa fiti timu pinzani zitateseka.
LAKERS, WARRIORS
Timu hizo mbili ni ajabu kwamba kwenye vitabu vya utabiri wa kucheza fainali NBA, hazijapewa nafasi ya kufika kutokana na kutokuwa na mwendelezo bora wa matokeo kwenye ligi ndefu na mtoano.
Lakini hiyo siyo sababu ya kuziweka pembeni kama utabiri huo kwani zina uwezekano wa kushtua na kufanya lolote kama siyo kubeba kabisa taji hilo. Lakers inayoongozwa na LeBron akiwa na Anthony Davis inaweza kufanya makubwa kama mambo yatakwenda vyema bila kuumia kwa mastaa hao wawili ambapo mbali na kushinda taji 2020, bado ina njaa ya kulichukua tena.
Golden State Warriors nayo si haba ikiwa na uwepo wa Stephen Curry mwenye uwezo wa kuibeba. Timu hiyo inaweza kushtua na kuikuta fainali na hata kubeba kama ilivyoshtua 2022 ilipobeba dhidi ya Celtics waliokuwa wanapewa nafasi kubwa kushinda taji.
HIZI PIA ZIMO
Ukiachana na timu hizo zinazoweza kucheza fainali na kuzizuia Celtics na Mavericks kurudia fainali ya msimu uliopita, timu ambazo pia zinaweza kushtua na kucheza fainali ni Oklahoma City Thunder, Sacramento Kings, Los Angeles Clippers, Philadelphia 7ers na Miami Heat.