Azizi Ki, Ronaldo lolote litatokea

Muktasari:
- Amrabat, ambaye amejiunga na Wydad akitokea Hull City, alizungumza na tovuti ya The Telegraaf na kueleza kuwa timu hiyo ya Morocco inafanya jitihada za kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Ureno.
CASABLANCA, MOROCCO: KIUNGO wa zamani wa Yanga, Stephen Aziz Ki huenda akacheza timu moja na Ronaldo baada ya staa wa kimataifa wa Morocco, Nordin Amrabat kuthibitisha uvumi kuwa timu yake mpya, Wydad Casablanca, inafanya mazungumzo na wawakilishi wa Cristiano Ronaldo kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Amrabat, ambaye amejiunga na Wydad akitokea Hull City, alizungumza na tovuti ya The Telegraaf na kueleza kuwa timu hiyo ya Morocco inafanya jitihada za kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Ureno.
Amrabat anajiunga na klabu hiyo ya Morocco akitokea Hull City, na ataiwakilisha Wydad katika Kombe la Dunia la Klabu kuanzia mwezi ujao.
Katika mahojiano hayo, winga huyo aliweka wazi kuwa waajiri wake wapya wanazungumza na wachezaji wengi wakubwa na Ronaldo ni miongoni mwao.
Inaelezwa Ronaldo anatafuta nafasi ya kucheza michuano hii na Wydad inaamini inaweza kumpata kwa ajili ya ushiriki wao kwenye michuano hiyo.
Mkataba wa Ronaldo na Al-Nassr unakamilika Juni, 30, lakini Kombe la Dunia la Klabu linaanza Juni 12, hivyo ikiwa Wydad itahitaji saini yake italazimika kuuvunja mkataba wake ili iweze kumpata mapema.
“Rais wa klabu ana ndoto kubwa na bado anazungumza na majina makubwa. Ni kweli kwamba Cristiano ni mmoja wao.”
Al-Nassr wana mechi moja ya mwisho msimu huu, ambapo watacheza ugenini dhidi ya Al Fate, leo usiku na inaonekana kuna uwezekano mkubwa kuwa hii ndiyo itakuwa mechi ya mwisho ya Ronaldo akiwa na timu hiyo.
Aziz Ki amejiunga na Wydad wiki hii ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga ambapo mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.