Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bruna Biancardi ndiye kiboko wa Neymar Jr

Muktasari:

  • Wawili hao walipata mtoto wao wa kwanza Oktoba 2023 na kumpa jina la Mavie lakini mwezi mmoja baadaye Biancardi alitangaza kuwa wameachana bila kuweka wazi sababu ya kuchukua hatua hiyo iliyowashangaza wengi.

MSHAMBULIAJI  wa zamani wa FC Barcelona na Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr, 32, amewahi kuhusishwa na warembo kadhaa ila mwanamitindo wa nyumbani kwao, Bruna Biancardi, 30, ndiye kiboko yake katika panda shuka walizopitia.

Wawili hao walipata mtoto wao wa kwanza Oktoba 2023 na kumpa jina la Mavie lakini mwezi mmoja baadaye Biancardi alitangaza kuwa wameachana bila kuweka wazi sababu ya kuchukua hatua hiyo iliyowashangaza wengi.

“Hili ni suala la kibinafsi zaidi lakini ninaposhughulika habari za kusadikika na utani wa kila siku, ninawajulisha kuwa sipo katika uhusiano na Neymar, sisi ni wazazi wa Mavie, na hiyo ndiyo sababu ya uhusiano wetu,” alisema Biancardi kupitia Instagram.

Utakumbuka Neymar kutokea Brazil anayekipiga Al Hilal SFC inayoshiriki Saudi Pro League, hadi sasa ni baba wa watoto watatu kutoka kwa wanawake tofauti, kuna Davi Lucca da Silva Santos (2011), Mavie (2023) na Helena (2024).  

Lakini mpenzi huyu wa Neymar ni nani hasa na kwanini ndiye kiboko yake? Biancardi, mzaliwa wa Brazil, amejipatia umaarufu katika tasnia ya mitindo akifanya kazi na lebo kadhaa za wabunifu zikiwamo Louis Vuitton, Off-White na Balmain.

Akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 12.2 kwenye Instagram, Biancardi anatengeneza sana maudhui ya mitindo na urembo akiwa na programu yake inayofamika kama ‘Get Ready With Me’ ambayo inalenga kukuza uelewa kuhusiana na tasnia hiyo.

Mbali na kazi hiyo yeye ni mtu wa kusafiri sana, ikiwa hahudhurii wiki ya mitindo au mafunzo ya utengenezaji wa filamu, Biancardi anaweza kupanda ndege na kwenda kokote duniani kuanzia Maldives, Qatar, Dubai na Italia.

Kipindi Neymar bado anakipiga pale PSG, mabingwa wa Ligue 1 mara 12, Biancardi alimtembelea mara kwa mara akitokea kwao Brazil na mara nyingi aliweka mafanikio ya ziara zake Paris nchini Ufaransa katika ukurasa wake wa Instagram.

Huyu pia ni rafiki wa mke wa Lionel Messi, Antonela Roccuzzo, mfano Februari 2023, Biancardi alichapisha mtandaoni mfululizo wa picha zake na kundi la wanawake akiwamo na Roccuzzo na wenzi wengine kadhaa wa wanasoka.

Awali, mnamo Agosti 2021, The Sun waliripoti kuwa Biancardi alijumuika na Neymar, Messi, Roccuzzo na mastaa wengine kwa ajili ya kupata chakula cha usiku huko Ibiza na ndio ulikuwa mwanzo wa uhusiano wao ingawa hawakutaka kuthibitisha.

Ikumbukwe Neymar na Messi walicheza pamoja Barcelona ya Hispania kuanzia mwaka 2013 hadi 2017, mastaa hao kutokea Amerika Kusini walikuwa karibu sana kipindi hicho hadi kutambulishana wapenzi wao ambao nao walikuja kuwa marafiki.

Uhusiano wa wawili hao uliwekwa hadharani Aprili 15, 2022 baada ya wote kuchapisha picha Instagram walizopiga katika birthday ya Biancardi wakiwa na marafiki na familia kwa ujumla ingawa awali walichagua kuweka mapenzi yao nje ya mitandao.

Hata hivyo, ndani ya mwaka huo huo waliachana, kufikia Februari 2023, Biancardi alimtakia Neymar heri ya kuzaliwa kupitia Instagram kwa kuchapisha picha yao wakipigana busu, hivyo kuthibitisha kwamba walikuwa wamerudiana.

“Leo nimekuambia kila kitu, ninaweka picha hii hapa kwa ajili ya kumbukumbu tu. Mwaka wako mpya uwe wa baraka!, usikose sababu za kusherehekea marafiki, mafanikio na afya, Mungu aendelee kuulinda uhusiano wetu,” alisema Biancardi.

Na kweli walikuwa wamerudiana kikamilifu, namaanisha Aprili 2023 walitangaza kutarajia mtoto wao kwanza ila akiwa ni wa pili kwa Neymar ambaye tayari alishapata mtoto na Carolina Dantas alipokuwa na umri wa miaka 19.

“Tunaota kuhusu maisha yako, tunapanga mengi kuhusu kuwasili kwako, na tunajua kwamba uko hapa ili kukamilisha mapenzi yetu na kufanya siku zetu kuwa za furaha zaidi,” aliandika Neymar kwenye Instagram katika picha iliyomuonyesha akilibusu tumbo la Biancardi.

“Utafikia katika familia nzuri, kaka yako, babu, bibi, wajomba na shangazi zako tayari wanakupenda sana! Njoo haraka mwanangu, binti yangu, tunakungoja kwa hamu!,” alieleza Neymar. 

Miezi miwili baadaye, Neymar na Biancardi walifanya tafrija ya kuweka wazi jinsi ya mtoto ambapo walithibitisha kuwa wanatarajia kupata mtoto wa kike waliyemtaja kama zawadi kuu.

“Tuna shauku kubwa ya kukutana nawe ana kwa ana, binti yangu wewe ni zawadi yetu kuu!,” alisema Biancardi ambaye alikuja kujifungua Oktoba 6, 2023 na kumpa mtoto wake jina la Mavie likiwa na maana ya ‘maisha yangu’ kwa Kireno.

“Mavie wetu amewasili salama katika maisha yetu. Karibu, binti! Tayari unapendwa sana na sisi... asante kwa kutuchagua kuwa wazazi wako,” Biancardi na Neymar waliandika Instagram wakiambatanisha na picha nyingi za mtoto mchanga.

Ila mwezi mmoja baada ya hapo waliachana! Kumbe Neymar alikuwa na uhusiano mwingine na Larissa Kimberlly. Chini ya miezi tisa baada ya kuzaliwa kwa Mavie, Neymar na Kimberlly wakapata mtoto wa kike Helena aliyezaliwa Julai 3, 2024.

Licha ya kwenda kwa Kimberlly, Neymar alijikuta akirudi tena kwa Biancardi baada ya mwaka mmoja, inaonekana kwa bibie hana ujanja, ndiye kiboko yake kama alivyoimba Alikiba katika wimbo wa Mwana FA, Kiboko Yangu (2014).

“Kwa sifa moja umenikamata, nakupa wewe peke yako ndio umeniweza. Nilikupita nimeteleza, lakini kwako, wewe ndio kiboko yangu,” Alikiba katika wimbo huo ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2015 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana.

Na Oktoba 2024, ndipo Neymar alithibitisha kurudiana na Biancardi ingawa mwezi mmoja kabla mrembo huyo aliweka wazi kupitia Instagram kuwa alionana na mchezaji huyo huko Dubai na ndipo tetesi za kurudiana zikaanza na hadi sasa wapo pamoja kama familia.