Bilbao yaikazia Madrid kwa Nico Williams

Muktasari:
- Williams ni miongoni mwa wachezaji ambao Madrid inadaiwa kutaka kuwasajili katika dirisha hili baada ya wapinzani wao Barcelona kujiondoa katika mazungumzo juu ya dili la staa huyo mwenye umri wa miaka 22.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Athletic Bilbao, Ernesto Valverde ametuma ujumbe kwa Real Madrid, baada ya kusisitiza kuwa mabosi wa timu hiyo wanafanya kila linalowezekana ili staa wao Nico Williams abakie kwenye kikosi chao kwa msimu ujao.
Williams ni miongoni mwa wachezaji ambao Madrid inadaiwa kutaka kuwasajili katika dirisha hili baada ya wapinzani wao Barcelona kujiondoa katika mazungumzo juu ya dili la staa huyo mwenye umri wa miaka 22.
Williams alisaini mkataba mpya na Bilbao katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini anaweza akaondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Euro 58 milioni.
Valverde anaamini kuwa Williams atasalia Bilbao, akisema mchezaji huyo ni "mwenye furaha sana", na timu inataka abaki.
Msimu huu Bilbao imekuwa katika kiwango bora sana inaonekana kuwa karibu kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao, kwa sasa wakiwa wanashikilia nafasi ya nne kwa pointi zao 70.
Mabosi wa Bilbao wanaamini ikiwa watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao inaweza kuwasaidia kama sehemu ya ushawishi wa kumbakisha kiungo huyu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Valverde alisema: "Tunadhani atakuwa nasi msimu ujao, na tunataka iwe hivyo. Daima kunakuwa na uvumi kuhusu wachezaji, na mnajua hali ilivyo. Tumeridhika sana na Nico, na Nico ameridhika sana kuwa nasi. Tunatumai kuwa mwaka ujao utakuwa mwaka mzuri kwa Nico, na atakuwa na sisi hapa."
Williams alicheza mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Barcelona wikiendi iliyopita na kiujumla amemaliza ligi akiwa amefunga mabao 11 katika mechi 44 za michuano yote.