Bila Toney Arsenal haibebi ubingwa

LONDON, ENGLAND. MKONGWE wa Arsenal Ian Wright amesema timu hiyo itashindana na Manchester City katika mbio za ubingwa endapo itamsajili straika wa Brentford Ivan Toney katika dirisha dogo la usajili la Januari.
Arsenal ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England tofauti ya pointi mbili dhidi ya Man City baada ya kuifunga wikiendi iliyopita.
Hiyo ni hatua nzuri kwa kocha Mikel Arteta kutokana na ushindi huo wa kwanza Ligi Kuu England dhidi ya Man City tangu mwaka 2015.
Lakini mkongwe huyo amedai Arsenal inatakiwa kufanya usajili wa straika mpya ambaye ataongeza nguvu katika kikosi na kumpendekeza Toney.
Akaongeza kuwa Arsenal haitafika mbali ikiendelea kumtegemea Eddie Nketiah na Gabriel Jesus ambao sio hatari zaidi wanapokuwa eneo la hatari.
"Tulipoteza mabao mengi na ikatuweka katika nafasi fulani. Nadhani Toney atafaa zaidi kwa sababu ni mchezaji anayejua kufunga. Ukizungumzia Nketiah na Jesus utarudi nyuma katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham, Jesus alikosa mabao mengi sana, kwa mchezaji mwenye uwezo kama Jesus maeneo kama yale jitihada inahitajika zaidi."
Martinelli na Martin Odegaard walikuwa wafungaji bora wa Arsenal msimu uliopita kwani kila mmoja alifunga mabao 15 wakiwazidi Nketiah na Jesus.
Toney ambaye amehusishwa na Arsenal alifunga Brentford mabao 20 msimu wa 2022-23 lakini anakibiliwa na adhabu ya kufungiwa miezi nane baada ya kukiri kuwa anabeti. Straika huyo wa kimataifa wa England atarejea Januari kuendelea na maisha yake ya soka.