Bellingham kupasuliwa bega

Muktasari:
- Real Madrid ambayo msimu huu imepoteza taji la La Liga kwa Barcelona, inashiriki Kombe la Dunia la Klabu itakayofanyika kuanzia Juni 14 hadi Julai 13 mwaka huu nchini Marekani.
MADRID, HISPANIA: NYOTA wa Real Madrid, Jude Bellingham anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa bega baada ya mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu, hatua ambayo huenda ikamweka nje ya uwanja kwa miezi kadhaa.
Real Madrid ambayo msimu huu imepoteza taji la La Liga kwa Barcelona, inashiriki Kombe la Dunia la Klabu itakayofanyika kuanzia Juni 14 hadi Julai 13 mwaka huu nchini Marekani.
Bellingham anatarajiwa kuwamo kwenye kikosi cha Madrid kitakachosafiri kwenda kushiriki mashindano hayo. Hata hivyo, atakuwa akicheza huku bado akiwa na majeraha aliyoyapata mwaka 2023 baada ya kuumia kwa kuanguka vibaya na kuvunjika bega.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, alikataa kufanyiwa upasuaji mwanzoni mwa msimu na ameendelea kucheza akiwa na jeraha hilo kwa misimu miwili mfululizo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka The Athletic, Real Madrid sasa ina mpango wa kumpeleka Bellingham kwenye upasuaji mara baada ya mashindano ya Kombe la Dunia la Klabu kukamilika.
Upasuaji huo unaweza kumuweka nje kwa takriban wiki 12, jambo ambalo linamaanisha kiungo huyo huenda akakosa mwanzo wa msimu wa 2025-26 wa La Liga.
Bellingham alianza vizuri msimu wa kwanza ndani ya Madrid aliyojiunga nayo Julai 2023 kutoka Borussia Dortmund kwa Pauni 115 milioni.
Katika msimu huo wa kwanza, Madrid ilitwaa ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya huku Bellingham akifunga mabao 23 katika mechi 43.
Lakini msimu huu ambao ni wa pili kwake, amefunga mabao 14 katika mechi 51, huku Madrid ikipoteza taji la La Liga na kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Arsenal.
Madrid pia ilifungwa 3-2 na Barcelona katika fainali ya Kombe la Mfalme (Copa del Rey), mechi ambayo Bellingham alikuwa miongoni mwa wachezaji watatu waliotolewa kwa kadi nyekundu.
Kwa msimu ujao, Bellingham anatarajiwa kuungana na nyota mwenzake wa timu ya taifa ya England, Trent Alexander-Arnold ambaye hajaongeza mkataba na Liverpool akikaribia kutua Real Madrid.
Madrid inataka Trent awepo kikosini kwao kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la Klabu na huenda ikailipa Liverpool ada ndogo ya karibu pauni milioni 1 ili kufanikisha uhamisho huo mapema.