Bayer Leverkusen ndoo hii hapa!

Muktasari:

  • Klabu hiyo tangu imeanzishwa mwaka 1904, haijawahi kutwaa ubingwa wa Bundesliga wala taji lolote kubwa hadi kufikia kupachikwa jina la kebehi la ‘Neverkusen’ yaani kutwaa ubingwa kwao ni ‘never’ (kamwe).

MUNICH, UJERUMANI: Wikiendi ya ubingwa imewadia. Bayer Leverkusen inaweza kuandika historia mpya wikiendi hii kwa kutwaa ubingwa wa Bundesliga kwa mara ya kwanza katika miaka 120 ya kuasisiwa kwa klabu hiyo itakapoikaribisha Werder Bremen kwenye Uwanja wa BayArena kesho.

Klabu hiyo tangu imeanzishwa mwaka 1904, haijawahi kutwaa ubingwa wa Bundesliga wala taji lolote kubwa hadi kufikia kupachikwa jina la kebehi la ‘Neverkusen’ yaani kutwaa ubingwa kwao ni ‘never’ (kamwe).

Jina hilo lilitokana na klabu hiyo kumaliza ya pili mara tano katika Bundesliga na kuwa timu pekee ambayo imemaliza ya pili mara nyingi zaidi bila ya kutwaa ubingwa Ulaya.

Leverkusen pia ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2002 na licha ya kikosi chake kuundwa na wakali kama Michael Ballack, beki tano Mbrazili Lucio na straika Dimitar Berbatov, ilikufa 2-1 mbele ya Real

Madrid, Zinedine Zidane akifunga bao lile la kihistoria alipounga juu kwa juu krosi ya beki Roberto Carlos. Timu hiyo pia ilipoteza fainali tatu za DFB na hivyo kuonekana ni timu ambayo “kamwe” haiwezi kutwaa taji.

Mataji pekee ambayo Leverkusen imewahi kushinda ni UEFA Cup 1987/88 na DFB Cup 1992/93.

Lakini kocha Xabi Alonso na jeshi lake kesho wanaweza kumaliza unyonge huo watakapoikaribisha nyumbani Werder Bremen kwa sababu wakishinda watakuwa mabingwa.

Leverkusen imekuwa na msimu bora sana 2023-24 kwani mbali ya kubakisha pointi 3 tu kutwaa ndoo ya Bundesliga, pia imetanguliza mguu mmoja kwenye nusu fainali ya Europa League baada ya kushinda nyumbani 2-0 dhidi ya West Ham usiku wa kuamkia jana kabla ya mechi yao ya marudiano itakayopigwa ugenini England Alhamisi ijayo.

Baada ya kuipoteza West Ham kwa kuipigia mashuti 13 yaliyolenga lango dhidi 1 na kumiliki mpira kwa asilimia 73 dhidi ya 27 za Hammers, Leverkusen sasa imeendeleza rekodi ya kucheza mechi 42 bila ya kupoteza katika michuano yote msimu huu wa 2023/24.

Mabingwa watetezi Bayern Munich ambao wamelishikilia taji la Bundesliga kwa misimu 11 mfululizo, wanajiandaa kulitema kwa mara ya kwanza wakiwa katika nafasi ya pili na pointi zao 60, sawa na VfB Stuttgart, kila timu ikicheza mechi 28.  Bayern iko hatarini kupoteza hata nafasi ya pili kwa Stuttgart kama itaendelea kuvurunda. Ila leo inawaalika vibonde FC Cologne wanaoshika nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 22.

RB Leipzig na Borussia Dortmund zilizo katika nafasi ya nne na ya tano mtawalia zikiwa na pointi 53 kila moja, zinaendelea kugombea kumaliza ndani ya Top 4 ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.