Barcelona yamgeukia Diaz baada ya Nico

Muktasari:
- Awali Barca ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili, Nico ambaye hata yeye alitamani sana kujiunga nao kwa mujibu wa ripoti lakini changamoto inadaiwa kuwa ni timu hiyo haikumhakikishia nafasi ya kuingiza jina lake katika mfumo moja kwa moja kutokana na kanuni za kifedha za La Liga.
BARCELONA imepanga kuhamishia nguvu zao zote kwenye mchakato wa kumsajili winga Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz mwenye umri wa miaka 28, baada ya kufeli kumpata staa wa Athletic Bilbao Nico Williams.
Awali Barca ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kumsajili, Nico ambaye hata yeye alitamani sana kujiunga nao kwa mujibu wa ripoti lakini changamoto inadaiwa kuwa ni timu hiyo haikumhakikishia nafasi ya kuingiza jina lake katika mfumo moja kwa moja kutokana na kanuni za kifedha za La Liga.
Nico aliiambia Barca kuwa hataki kimtokee kile kilichomtokea Dani Olmo msimu uliopita ambapo alisimamishwa kwa muda kucheza baada ya La Liga kumwondoa katika usajili kwa sababu uwepo wake ulisababisha matumizi ya Barca kuwa makubwa tofauti na kile walichokuwa wameingiza jambo ambalo ni kinyume na kanuni.
Sasa Barca inahamishia nguvu za Diaz ambaye mara kadhaa amewahi kuripotiwa kuwa kucheza Barcelona ni ndoto yake.
Giorgio Scalvini
NEWCASTLE United imemuweka mchezaji wa kimataifa wa Italia anayeichezea Atalanta, Giorgio Scalvini, katika kipaumbele cha wachezaji inaohitaji kuwasajili katika dirisha hili ili kuboresha eneo lao la uzuiaji.
Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 21, anauzwa kwa kiasi kisichopungua pauni 30 milioni. Mkataba wake wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Viktor Gyokeres
KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, ameweka muda wa chini ya wiki mbili kwa timu hiyo kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, mwenye umri wa miaka 27.
Arteta ametoa muda huo ili kuhakikisha anasajili mshambuliaji wa kati kwa haraka na kuanza naye maandalizi ya msimu.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 27, naye bado anawindwa na Barcelona ambayo sasa imewaweka katika rada zake mastaa kibao katika dirisha hili ili kuboresha safu yao ya ushambuliaji.
Barca imezidisha juhudi kwa ajili ya kumpata Rashford kwa sababu inaamini itampata kwa bei rahisi zaidi.
Wojciech Szczesny
KIPA wa kimataifa wa Poland, Wojciech Szczesny, 35, anatarajiwa kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuendelea kusalia katika viunga vya Barcelona baada ya ule wa awali kumalizika.
Szczesny alisaini mkataba na Barca Oktoba mwaka jana akirejea baada ya kustaafu.
Barca ilimchukua fundi huyu kama mbadala baada ya Marc Andre ter stegen kupata majeraha ambayo yalimweka nje kwa muda mrefu.
Idrissa Gueye
KIUNGO wa Everton na timu ya taifa ya Senegal, Idrissa Gueye, 35, ambaye mkataba wake na timu hiyo ulimalizika Jumatatu, sasa amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja wenye chaguo la kuongeza mwaka mwingine ikiwa Everton itavutiwa na kiwango chake.
Kabla ya kusaini Idrissa alitajwa kuwa huenda angeondoka na kutimkia Saudi Arabia ambako timu kadhaa zilimhitaji.
Moise Kean
NAPOLI imeingia katika vita dhidi ya Manchester United na Al-Qadsiah ya Saudi Arabia kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Fiorentina na timu ya taifa ya Italia, Moise Kean, 25, katika dirisha hili.
Mkataba wa sasa wa Kean unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, na kuna kipengele ambacho kinamwezesha kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa euro 52 milioni, lakini kitamalizika Julai 15.
Lionel Messi
MABOSI wa Inter Miami bado wako katika mazungumzo na wawakilishi wa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 38, Lionel Messi, kuhusu kuongeza mkataba wake wa sasa unaomalizika mwishoni mwa Desemba mwaka huu.
Ripoti zinaeleza Messi yupo tayari kuendelea kusalia katika timu hiyo kwani bado anaamini ana kitu cha kuongeza.