Man united, Thomas Muller aje au asije?

Muktasari:
- Muller alisema amekuwa akivutiwa sana na Man United kwa muda mefu katika maisha yake ya soka, lakini amegoma kuweka wazi kama maneno hayo yanakwenda na mpango wa kuhamia kwenye klabu hiyo ya Old Trafford katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
FLORIDA, MAREKANI: AJE au asije? Pengine hilo ni swali wanalojiuliza mashabiki wa Manchester United kwa sasa baada ya staa wa Ujerumani na Bayern Munich, Thomas Muller kudai amekuwa akivutiwa na miamba hiyo ya Old Trafford kwa miaka mingi.
Muller alisema amekuwa akivutiwa sana na Man United kwa muda mefu katika maisha yake ya soka, lakini amegoma kuweka wazi kama maneno hayo yanakwenda na mpango wa kuhamia kwenye klabu hiyo ya Old Trafford katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Staa huyo ataachana na Bayern Munich wakati wa fainali za Kombe la Dunia la Klabu zitakapomalizika, hivyo yupo sokoni kutafuta klabu mpya. Na wakati huu akijaribu kwenda kujaribu bahati yake ng’ambo ya Ujerumani, fowadi huyo veterani alisema hakutakuwa na muunganiko mzuri kwake na klabu ya Man United endapo kama atatua Old Trafford kwa sasa.
Akizungumza na CBS Sports, Muller aliulizwa: “Hivi kuna ligi yoyote ya Ulaya ambayo uliwahi kuwaza kwa kusema ‘ningependa kucheza kwenye Ligi Kuu England au ?”
Alijibu: “Ndiyo, niliwaza sana juu ya hilo. Kuna nyakati nilisema, ‘Ok, pengine sasa ni kipindi mwafaka kwenye kupata uzoefu wa huko.”€
Muller kisha aliulizwa “Je, Manchester United ulishawahi kuifikiria?” Fowadi huyo veterani alijibu: “Mara nyingi. Au unamaanisha sasa hivi? Hapana, kwa sasa mimi sio mtu sahihi kwao na pia haitakuwa klabu sahihi kwangu..”€
Timu ya Muller, Bayern baada ya kukwama kwenye usajili wa staa wa Liverpool, Luis Diaz sasa imehamishia mpango kwenye mpango wa kumchukua Marcus Rashford, ambaye amefungua milango ya kutoka nje ya England baada ya kufutwa na kocha Ruben Amorim kwenye mipango yake Man United.
Rashford, 27, alionekana kurejea kwenye kiwango chake alipokuwa kwa mkopo Aston Villa, lakini kocha Unai Emery amegoma kumchukua jumla mchezaji huyo na hivyo kumrudisha Old Trafford.
Na kwenye kikosi cha Man United, kocha Amorim ameshamsajili Matheus Cunha kutoka Wolves huku akimfukuzia pia winga wa Brentford, Bryan Mbeumo, ili kuwa na sura tofauti kabisa katika safu ya ushambuliaji, ambapo miamba hiyo ya Old Trafford, ikiwa sokoni pia kusaka huduma ya straika mpya, ambapo moja ya majina yaliyopo ubaoni ni la mkali wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres. Man United itaanza mazoezi Jumatatu, Julai 7, ambapo mechi yake ya kwanza ya kirafiki itakipiga na Leeds United huko Stockholm, Sweden Julai 19. Baada ya hapo itakwenda Marekani kwenye kambi ya mazoezi, ambako itacheza mechi tatu dhidi ya West Ham, Bournemouth na Everton kabla ya kurudi Old Trafford kukabiliana na Fiorentina wiki moja kabla ya Ligi Kuu England kuanza.