Ayton ni suluhisho la ulinzi Lakers?

Muktasari:
Hatua hiyo imekuja baada ya Portland kukubali kuununua mkataba wake kwa zaidi ya Dola 25 milioni.
CALIFORNIA, MAREKANI:TIMU ya Los Angeles Lakers imefanikiwa kutimiza moja ya malengo yake makubwa ya dirisha la usajili baada ya kufikia makubaliano na Deandre Ayton, aliyekuwa mchezaji wa Portland Trail Blazers, kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine msimu wa 2026-27.
Hatua hiyo imekuja baada ya Portland kukubali kuununua mkataba wake kwa zaidi ya Dola 25 milioni.
Taarifa hizo zimethibitishwa na vyanzo viwili vya karibu na mazungumzo baina ya pande hizo, ambavyo vilizungumza kwa sharti la kutotajwa kutokana na taratibu za ligi kuruhusu kutangazwa baadaye.
Kwa Lakers, huo ni usajili wenye uzito wa kimkakati, kwani Ayton ambaye alichaguliwa nafasi ya kwanza kwenye NBA Draft 2018 - nafasi mbili mbele ya Luka Doncic sasa anajiunga na mpinzani wake wa muda mrefu ndani ya timu moja, wakiongozwa na mkongwe LeBron James.
LENGO LA USAJILI
Msimu uliopita ulikuwa mgumu kwa Lakers, hasa katika eneo la ulinzi na ushindani wa 'rebounds' baada ya kumuuza Anthony Davis kwenda Dallas. Upungufu uliiumiza timu hiyo hasa kwenye mechi za mchujo ambapo ilitolewa raundi ya kwanza na Minnesota Timberwolves ndani ya michezo mitano. Katika mchezo wa mwisho wa mfululizo huo, nyota wa Wolves Rudy Gobert aliweka rekodi ya 'double-double' ya pointi 27 na 'rebounds' 24 dhidi ya safu dhaifu ya Lakers. Kocha mpya JJ Redick alilazimika kumuweka benchi Jaxson Hayes kutokana na kushindwa kuhimili presha.
Hii ilionyesha kuwa timu hiyo inayohitaji mchezaji mwenye urefu, nguvu na uwezo wa kushindana eneo la 'paint' - hitaji ambayo Deandre Ayton anayatimizia kwa kiwango kikubwa.
NINI LAKERS WANAAMBULIA KWA AYTON
Ayton ni mchezaji mwenye urefu wa futi 7, uzito wa kilo 113 na uzoefu wa misimu saba NBA. Takwimu zake zinasomeka vyema wastani wa pointi 16.4, rebounds 10.5 na asilimia 59 ya maitupo inayowafikia walengwa.
Licha ya kukumbwa na majeraha msimu uliopita, Ayton ana rekodi ya kuwa mchezaji pekee tangu Dwight Howard kufanikisha 'double-double' kwa misimu saba mfululizo ya mwanzo NBA. Uwepo wake utaongeza urahisi kwa LeBron James na Luka Doncic kutumia mipira ya juu (lobs), kumiliki mpira katika sekunde za mwisho za mashambulizi.
Licha ya Ayton kutojulikana kama mlinzi kiongozi kama Gobert au Davis, ana uwezo mkubwa wa kumiliki vyema eneo la ulinzi na ni mzuri katika kuwapunguza wapinzani karibu na eneo la hatari.
BAHAMAS HADI CALIFORNIA
Ayton alizaliwa Bahamas, lakini alihamia San Diego, California akiwa na umri wa miaka 12 kwa ajili ya kuboresha kipaji chake katika shule ya sekondari. Aling’ara katika Chuo Kikuu cha Arizona kabla ya kuchaguliwa kuwa chaguo la kwanza na Phoenix Suns 2018.
Akiwa na Suns, Ayton aliisaidia kufika fainali ya NBA 2021, lakini mvutano kati yake na menejimenti ya Phoenix ulichangia kuhamia Portland miaka miwili baadaye kupitia dili la timu tatu lililompeleka Damian Lillard huko Milwaukee.
Katika kipindi chake Portland, Ayton alionekana kupotea kwenye mfumo wa timu inayojengwa upya, huku akicheza mechi 40 pekee msimu uliopita kabla ya kuumia mguu wa nyuma mwezi Februari. Hata hivyo, kiwango chake kilibaki thabiti na sasa anapata nafasi ya kufufua jina lake katika jukwaa la NBA akiwa na Lakers.