Arteta kupitisha fagio Arsenal

ARSENAL imepanga kupitisha fagio kusafisha mastaa isiokuwa na mpango nao mwishoni mwa msimu huu huku orodha hiyo ikidai kuwahusu pia straika Alexandre Lacazette na kiungo Matteo Guendouzi.

Huo ni mpango wa kocha Mikel Arteta anayejaribu kuondoa wachezaji ambao wanaoongeza wingi tu kwenye kikosi ili kupunguza bili ya mishahara na kuzalisha pesa nyingi kwa ajili ya kusajili wapya.

Kwenye dirisha la kiangazi la mwaka jana, Guendouzi, Lucas Torreira na Henrikh Mkhitaryan aliwaondoa kwenye kikosi chake kwa mkopo licha ya wengine kuhama jumla.

Na dirisha lililopita la Januari, fagio hilo liliendelea kwa Mesut Ozil, Shkodran Mustafi na Sokratis Papastathopoulos ambao walifunguliwa mlango wa kutokea, wakiruhusiwa kuondoka bure kabisa.

Arteta mwenyewe anafahamu kikosi anachotaka kukijenga katika chama hilo la Emirates, akitaka kuwa na wachezaji ambao watakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa timu huku akitaka kufanya usajili wake mwenyewe.

Kwa mujibu wa The Sun, kuna wachezaji wenye hadhi kubwa sana watafunguliwa mlango wa kutokea mwisho wa msimu na hilo linaweza kuwahusu David Luiz na Lacazette, ambao wamekuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza - huku beki wa Kibrazili mkataba wake ukifika tamati mwishoni mwa msimu huu na mwingine, straika wa Kifaransa, amepoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Wachezaji Guendouzi na Torreira, ambao kwa sasa wapo kwa mkopo Hertha Berlin na Atletico Madrid mtawalia. Mpango ni kupunguza bili ya mishahara.

Kwa kuwaondoa Ozil na Mustafi timu hiyo ilipunguza kiasi kikubwa cha mshahara kwenye kikosi chake na kupata nafuu kutokana na timu kutokuwa na mapato ya viingilio vya mashabiki huku ikikabiliwa pia na deni la Pauni 120 milioni kutoka kwenye Benki ya England, ambalo linatakiwa kulipwa.

Sead Kolasinac, Ainsley Maitland-Niles na Joe Willock ni wachezaji wengine waliotolewa kwa mkopo mwezi uliopita na kufanya timu hiyo iwe imeokoa Pauni 16.5 milioni za mishahara kutoka sasa hadi mwisho wa msimu.

Mshambuliaji Lacazette amepoteza nafasi kwenye kikosi cha Arteta, ambaye kwa sasa anawafikiria zaidi Pierre-Emerick Aubameyang, Bukayo Saka na Emile Smith Rowe.

Atletico Madrid imekuwa ikihusishwa na Lacazette, huku Juventus nao wakihitaji mshambuliaji huyo sambamba na AS Monaco. Lacazette yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake unaomshuhudia akilipwa Pauni 150,000 kwa wiki.