Mbappe awatoa kwenye ramani Ronaldo, Messi

Friday February 19 2021
mbape pic

PARIS, UFARANSA

DOGO anajua. Kylian Mbappe mavitu yake ya ndani ya uwanja ni bora kuliko masupastaa wawili moto, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakati walipokuwa na umri kama wake, huku akipagawisha mashabiki wa soka kutokana na kiwango chake alichoonyesha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumanne iliyopita.

Kinda huyo wa Paris Saint-Germain alikuwa nyota wa mchezaji wakati alipoichachafya Barcelona ya Messi na kufunga hat-trick, timu yake ikishinda 4-1 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 ya mtoano uliofanyika uwanjani Nou Camp.

Mabao yake hayo matatu yamemfanya afikishe mabao 24 kwenye michuano hiyo ndani ya mechi 41 tu, huku akipiga asisti 16 katika mechi hizo.

Katika umri sawa wa miaka 22 na siku 58, Messi alikuwa amefunga mabao 17 na kuasisti mara saba huku akiwa amecheza mechi 33 kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi cha Barca.

Kwa upande wa Ronaldo, kwenye umri huo alikuwa bado hajafunga bao lolote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, licha ya kwamba alikuwa amecheza mechi 26 za michuano hiyo akiwa na Manchester United.

Advertisement

Ilimchukua mechi 30, Ronaldo kufunga bao lake la kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo alifunga mara mbili kwenye ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya AS Roma, Oktoba 2007.

Mbappe, ambaye hadi sasa ameshafunga mabao 16 katika michuano yote aliyocheza msimu huu kwenye kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino, bado ana safari ndefu ya kufikia rekodi ya jumla ya miamba hiyo miwili ya soka kwenye mabao.

Ronaldo, 36, amefunga mabao 134 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akishinda ubingwa mara tano, akisaka jingine akiwa na kikosi cha Juventus, ambapo usiku wa juzi Jumatano alikwenda kuwakabili FC Porto kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora.

Messi, 33, ndiye anayemkaribia Mreno huyo kwa mabao na mataji kwenye michuano hiyo, akifunga mara 119 na amebeba ubingwa huo mara nne. Licha ya mastaa hao wawili kushinda Ballon d’Or mara 11 kwa pamoja, staa wa zamani wa Ligi Kuu England, Joe Cole kwa shughuli ya Mbappe kwenye usiku huo wa Jumanne, anaamini kwa sasa ndiye mchezaji bora kuliko Ronaldo na Messi.

Kiungo huyo wa zamani wa England, Chelsea na West Ham United aliambia BT Sport: “Mbappe ni mchezaji bora kwa kipindi hiki.”

Rio Ferdinand aliamua kupoza makali kidogo kwa kucheza, Mbappe amechukua taji kutoka Messi na Ronaldo.

Beki huyo wa zamani wa Manchester United alisema: “Mbappe yupo yeye mwenyewe tu - nje ya wachezaji wengine vijana yupo yeye tu. Watu wanasahahu kwamba ana umri wa miaka 22.

“Hebu ona ameshinda Kombe la Dunia, ona anachofanya kwenye Ligi Kuu Ufaransa na kile anachofanya kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni balaa. Huyu jamaa amechukua taji kutoka kwa Messi na Ronaldo.”

TAKWIMU ZA MASTAA HAO

KWENYE UMRI WA MIAKA 22

*Kylian Mbappe

Umri: Miaka 22

Amecheza: Mechi 41

Ameanza: Mechi 34

Uwanjani: Dakika 3,086

Amefunga: Mabao 24

Amechangia: Asisti 16


*Lionel Messi

Umri: Miaka 22

Amecheza: Mechi 33

Ameanza: Mechi 28

Uwanjani: Dakika 2,452

Amefunga: Mabao 17

Amechangia: Asisti 7


*Cristiano Ronaldo

Umri: Miaka 22

Amecheza: Mechi 26

Ameanza: Mechi 23

Uwanjani: Dakika 1,987

Amefunga: Mabao 0

Amechangia: Asisti 5Advertisement