Arteta kasema... Arsenal ni bora

Muktasari:
- Arsenal imefungasha virago na kutupwa nje baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-1 na ilibaki ikilalamikia nafasi nyingi za mashambulizi ilizozipoteza kwenye mechi mbili dhidi ya PSG, ambazo ilipoteza zote, 1-0 uwanjani Emirates wiki iliyopita na 2-1 uwanjani Parc des Princes, Jumatano usiku.
LONDON, ENGLAND: MIKEL Arteta amedai kwamba Arsenal ilikuwa timu bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na ilikuwa vizuri kuliko Paris Saint-Germain licha ya kutupwa nje ya michuano hiyo kwenye hatua ya nusu fainali.
Arsenal imefungasha virago na kutupwa nje baada ya kuchapwa jumla ya mabao 3-1 na ilibaki ikilalamikia nafasi nyingi za mashambulizi ilizozipoteza kwenye mechi mbili dhidi ya PSG, ambazo ilipoteza zote, 1-0 uwanjani Emirates wiki iliyopita na 2-1 uwanjani Parc des Princes, Jumatano usiku.
Ukame wa kubeba taji kwa Arsenal sasa unafikia miaka mitano huku msimu huu ikimaliza mikono mitupu bila ya taji lolote, ikitoka kapa pia kwenye Ligi Kuu England, Kombe la Ligi na Kombe la FA. Kipa wa PSG, Gianluigi Donnarumma aliokoa hatari nyingi, wakati Declan Rice na Bukayo Saka walikosa nafasi nyingi.
Alipoulizwa baada ya mechi hiyo, Arteta alisema: “Sawa, kwanza nawapongeza PSG kwa kufika fainali. Kuhusu uchambuzi, nitafanya nikiwa nimetulia, lakini nilichokiona ni kwamba kwenye benchi letu kulikuwa na watu bora kuliko wao.
“Ukitazama mechi mbili, unaweza kuona mchezaji wao bora uwanjani alikuwa kipa. Yeye ndiye aliyeleta tofauti katika mechi. Nadhani tulikaribia kabisa, tulikaribia kuliko haya matokeo na bahati mbaya tumetolewa. Najivunia wachezaji wangu, kwa kile walichokifanya, walivyokabiliana na presha maana baada ya dakika 20, mambo yangeweza kuwa 3-0.”
Alipoulizwa kama kuna maendeleo yoyote kwa timu yake, Arteta alijibu: “Asilimia 100, sidhani kama kuna timu bota kwenye michuano hii kutuzidi. Tulichokifanya tulistahili la zaidi kwenye mechi zote mbili. Lakini, michuano hii ni kuhusu ndani ya boksi, mastraika na kipa, ambaye ndiye aliyekuwa mchezaji wao bora kwenye mechi zote mbili.”
Arteta aliongeza: “Nimehuzunika. Tulikaribia kushinda kwenye mechi zote mbili. Tulikuwa bora zaidi yao. Lakini, hatupo fainali na hilo linaniuma kwa sababu kama unataka kushinda hii michuano inahitaji kufika huko. Tumetolewa, lakini mimi siangalii kwa namna hiyo.”
Hata hivyo, kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger ametofautiana na Arteta kuhusu madai yake kwamba walikuwa bora uwanjani kuliko PSG, akisema kwenye mechi zote mbili, mabingwa hao wa Ufaransa walicheza kwa mipango, hasa mechi ya pili waliwaacha Arsenal wabaki na mpira, lakini kitu ambacho walifanya ni kuwadhibiti wasitikise nyavu zao.