Arteta atoa tamko Arsenal

Tuesday April 06 2021
arsenal pic

LONDON, ENGLAND

HUKU minong’ono ya hapa na pale ikiendelea kwenye mabasi mbali mbali ya usafiri wa umma jijini London juu ya kiwango kibovu cha Arsenal, kocha wa kikosi hicho Mikel Arteta ameibuka na kuwaomba msamaha mashabiki wa timu hiyo baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool, juzi, jumamosi.

Arteta alionekana kuwa mwenye hasira baada ya vijana wake kukubali kuruhusu mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool, na kusisitiza kwamba atakwenda kuongea na wachezaji hao ili wabadilike kwenye mchezo ujao wa Europa League dhidi ya Slavia Prague, Alhamisi hii.

Arsenal ilipoteza mechi hiyo licha ya kuanza na wachezaji wake watatu ghali zaidi zaidi kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa msimu huu.

Wachezaji hao ni pamoja na Alexandre Lacazette, Pierre-Emerick Aubameyang na Nicolas Pepe ambao wote kwa pamoja wameigharimu Arsenal Pauni 174.5 milioni kwenye usajili wao.

Hata hivyo, Arsenal ilikuwa inawakosa wachezaji wake waliowapandishwa kutoka kwenye akademi Emile Smith Rowe na Bukayo Saka ambao wameonekana kuwa na mchango mkubwa kutokana na viwango walivyoonyesha na kukosekana kwao kumetajwa kama sababu moja wapo ya kupoteza.

Advertisement

“Liverpool walistahili kushinda kwa sababu walikuwa bora kwenye kila idara, tunahitaji kuomba msamaha kwa mashabiki wetu, naweza kusema naomba msamaha sana kwa kile tulichofanya ndani ya uwanja na mimi ndio napaswa kuwajibika kwa sababu wao walikuwa bora zaidi yetu,” alisema Arteta na kuongeza: ”Waliunasa kila mpira tuliogombania nao, kikukweli ulikuwa ni mchezo tulioonyesha kiwango kibovu tangu nianze kuifundisha timu hii. Siwezi kuleta visingizio kwamba hatukuwa na wachezaji wetu watano sijui sita, sijali kuhusu nani alikosekana, kawaida huwa nachukia sana visingizio sababu ya kufungwa ni walikuwa bora sana kuliko sisi katika kila idara

“Kazi yangu kama kocha ni kuhakikisha kila mchezaji kwenye timu anacheza kwenye kiwango kinachotakiwa,” aliongeza.

Kipigo hicho kimesababisha Arsenal iendelee kusalia kwenye nafasi ya tisa ikiwa na pointi 42 baada ya kucheza mechi 30 huku timu iliyo juu yake ambayo ni Everton ina alama 46 ilizokusanya kwenye mechi 28.

Advertisement