Arsenal yatoa msimamo kwa Alexander Isak
Muktasari:
- Isak ambaye msimu huu ameonyesha kiwango bora tangu ulipoanza, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028.
MABOSI wa Arsenal hawana mpango wa kutoa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kumsajili straika wa Newcastle United na timu ya taifa ya Sweden, Alexander Isak, 25, katika dirisha hili la usajili wa majira ya baridi huko UIaya.
Isak ambaye msimu huu ameonyesha kiwango bora tangu ulipoanza, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2028.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Newcastle United inahitaji zaidi ya Euro 115 milioni ili kumuuza mchezaji huyo katika dirisha hili au lijalo la majira ya kiangazi ikiwa ni katika mpango wa kuboresha eneo la ushambuliaji.
Kiasi hicho cha fedha kitavunja rekodi ya usajili na atakuwa mmoja kati ya wachezaji ghali zaidi ndani ya England akiungana na mastaa kama Moises Caicedo, Enzo Fernandez, Jack Grealish na Declan Rice walipouzwa kwa klabu ambazo wanazichezea katika Ligi Kuu England. Tangu kuanza kwa msimu huu Isak amecheza mechi 22 za michuano yote, amefunga mabao 15 na kutoa asisti nne.
Bryan Mbeumo
MANCHESTER United imeungana na Arsenal katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Brentford na Cameroon, Bryan Mbeumo, 25, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili. Mbeumo ambaye msimu huu amecheza mechi 23 za michuano yote na kufunga mabao 13, anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kujiunga na Arsenal kutokana na upungufu uliopo eneo la ushambuliaji.
Ronald Araujo
JUVENTUS imemuweka beki wa kati wa Barcelona na Uruguay, Ronald Araujo, 25, katika orodha ya mastaa inaowapa kipaumbele cha kuwasajili katika dirisha hili. Araujo ambaye msimu huu amecheza mechi moja amekuwa katika wakati mgumu tangu kuanza kwa msimu kwa sababu ya majeraha yanyomwandama. Licha ya kurejea katika kikosi baada ya kuwa na majeraha alikuwa benchi kwa mechi mbili.
Tyrick Mitchell
ATLETICO Madrid inataka kumsajili beki wa pembeni wa Crystal Palace, Tyrick Mitchell, 25, katika dirisha hili baada ya kutuma wawakilishi kwenda kutazama mech kadhaa za msimu huu ambapo amecheza msimu huu. Nyota huyo wa kimataifa wa England huduma yake pia inahitajika na baadhi ya timu England. Mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Jonathan David
WAWAKILISHI wa mshambuliaji wa Lille, Jonathan David wanadaiwa kuwasili London kufanya mazungumzo na mabosi wa West Ham juu ya dili la mshambuliaji huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Tangu kuanza msimu huu, Jonathan mwenye umri wa miaka 24 amecheza mechi 28 za michuano yote na kufunga mabao 17.
Evan Ferguson
WEST Ham United imeanza mazungumzo na mshambuliaji wa Brighton, Evan Ferguson kwa ajili ya kumsajili katika dirisha hili ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji. Mbali ya Ferguson, West Ham United pia inatajwa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Wolvehampton na Korea Kusini, Hwang Hee-chan, 28, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Jhon Duran
PSG inadaiwa kuwa katika hatua nzuri kwenye mazungumzo na wawakilishi wa Aston Villa ili kuipata huduma ya mshambuliaji raia wa Colombia, Jhon Duran, 21, katika dirisha hili. Kwa mujibu wa taarifa PSG imepanga kumtoa Kolo Muani, 26, na pesa kidogo ili kufanikisha dili hilo. Mkataba wa Duran unaisha 2030.
Dean Huijsen
REAL Madrid inaripotiwa kutuma wawakilishi England kwa ajili ya kumtazama beki wa Bournemouth na Hispania, Dean Huijsen, 19, kabla ya kufikia mwafaka wa kutuma ofa ili kumsajili katika dirisha hili. Dean ambaye msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga mabao mawili, mkataba wake unamalizika 2030.