Ancelotti anatoka, Alonso anaingia

Muktasari:
- Alonso, 43, atajiunga na klabu hiyo ya zamani kwa mkataba wa miaka mitatu, akichukua mikoba ya Carlo Ancelotti, ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu huu.
MADRID, HISPANIA: MABOSI wa Real Madrid wanajiandaa kumtangaza kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso kuwa bosi mpya wa Bernabeu.
Alonso, 43, atajiunga na klabu hiyo ya zamani kwa mkataba wa miaka mitatu, akichukua mikoba ya Carlo Ancelotti, ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu huu.
Mabosi wa Bernabeu walikutana na Ancelotti siku ya pili baada ya kichapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka kwa Arsenal mwezi uliopita na hapo walikubaliana kila upande kuchukua njia zake.
Kocha huyo mkongwe wa Italia alishinda mataji mawili ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye awamu yake ya pili ya kuinoa klabu hiyo ya Madrid.
Real Madrid ilinyakua pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye awamu ya kwanza ya kocha Ancelotti huko Bernabeu.
Ancelotti, 65, alirejea Madrid mwaka 2021 na licha ya mafanikio yake, kukomea robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na kushindwa kufanya vizuri zaidi kwenye La Liga kumefanya zama zake kufika mwisho Bernabeu.
Marca linaripoti kwamba Ancelotti ataaga Bernabeu baada ya Madrid kucheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Real Sociedead. Alonso atakabidhiwa mikoba na atakuja na wasaidizi wake Sebas Parrilla na Alberto Encinas.
Alonso amekuwa akisakwa na timu nyingi baada ya kuiongoza Leverkusen msimu uliopita kubeba ubingwa wa Bundesliga bila ya kupoteza mchezo wowote. Msimu huu mambo yamekuwa magumu na taji hilo limebebwa na wapinzani wao, Bayern Munich.