Anazingua! Carragher hamtaki Trent Alexander- Arnold

Summary


LIVERPOOL, ENGLAND. MKONGWE wa Liverpool, Jamie Carragher ameuomba uongozi wa klabu hiyo isajili beki mwingine atakayemletea upinzani Trent Alexander-Arnold kwasababu anazingua kwasasa.

Kwa mujibu wa Carragher uwezo wa ukabaji wa beki huyo bado ni mdogo kwahiyo Liverpool inahitaji kufanya usajili wa nguvu msimu ujao.

Trent alionyesha kiwango kibovu kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya 16 bora ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid uliyochezwa uwanja wa Santiago Bernabeu, Liverpool iking'olewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-2.

Trent alicheza kwa mafanikio makubwa chini ya kocha Jurgen Klopp ndani ya misimu kadhaa iliyopita, lakini beki huyo ameonekana kuwa mwiba mchungu kwenye kikosi kutokana kiwango chake kushuka Liverpool ikiboronga msimu huu.

Licha ya Liverpool kung'oka sasa ipo katika hatihati ya kutofuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yatakayofanyika msimu ujao, majogoo wa jiji wameendelea kusuasua kwenye ligi na imejikita nafasi ya sita kwenye msimamo.

Akizungumza kwa hasira baada Liverpool kung'oka Carragher amekiri Tren anahitaji msaada kwasababu upande wake anaocheza umeonekana kuelemewa kwa asilimia kubwa.

"Nadhani muda umefika, Trent anahitaji mtu wa kumsaidia, amecheza kila wiki msimu yote ndani ya miaka minne iliyopita, nimepata hofu kuhusu kiwango chake, sio tu kwaajili ya Liverpool namaanisha timu nzima, isiendelee tena, kilichotokea msimu huu na mechi nyingi alizocheza kiwango chake kimeshuka, swali linakuja mchezaji gani ambaye watamsajili? nadhani imefikia kipindi Liverpool inatakiwa isajili beki mwingine, haijalishi watatoa bei gani, sio kama simpendi Trent hapana, namkubali sana ametoa mchango mkubwa, lakini kwasasa Trent anahitaji msaada," alisema Carragher

Carragher akaongeza akidai Trent anapata wakati mgumu kwasababu Liverpool ilipoteza mwelekeo msimu huu kutokana kiwango chao kibovu msimu huu. Kwasasa Liverpool ilichobakiza ni kupigania nafasi ya kufuzu Ligi Mabingwa Ulaya msimu huo kwa mujibu wa Carragher.