Amorim ana mtihani mwingine

Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Ureno, aliteuliwa kuchukua mikoba ya Erik ten Hag mapema mwezi huu na anatarajiwa kusimama katika benchi kwa mara ya kwanza Jumapili ya wiki hii ikiwa atapata kibali cha kazi.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester United, Ruben Amorim, huenda akapata wakati mgumu katika mchezo wake wa kwanza baada ya idadi ya majeruhi kuzidi kuongezeka.
Kocha huyo raia wa Ureno, aliteuliwa kuchukua mikoba ya Erik ten Hag mapema mwezi huu na anatarajiwa kusimama katika benchi kwa mara ya kwanza Jumapili ya wiki hii ikiwa atapata kibali cha kazi.
Man United inatarajiwa kukutana na Ipswich Town katika viunga vya Portman Road lakini itakuwa inakosa huduma za mabeki wao wengi kutokana na majeraha na hivi karibuni Victor Lindelof naye anadaiwa kuumia.
Lindelof ambaye aliichezea Sweden katika mchezo wao dhidi ya Slovakia Jumamosi jioni, hakumaliza hata kipindi cha kwanza baada ya kupata maumivu yaliyosababisha atolewe nje.
Alilazimika kusaidiwa kutoka uwanjani na wafanyakazi wawili wa matibabu wa Sweden na sasa inadaiwa kuwa majeraha yake yanaweza kumweka nje kwa muda.
Lindelof ni miongoni mwa mastaa ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutumika zaidi na Amorim kwa sababu alishamfundisha alipokuwa Benfica.