Rashford avuliwa jezi, apewa Cunha Man United

Muktasari:
- Man United imefichua kwamba Rashford ni miongoni mwa mastaa watano wa kikosi cha kwanza ambao wameiambia klabu wanataka kuhama dirisha hili la majira ya kiangazi.
MANCHESTER, ENGLAND: STAA wa Manchester United, Marcus Rashford amevuliwa jezi namba 10 na kukabidhiwa staa mpya, Matheus Cunha.
Man United imefichua kwamba Rashford ni miongoni mwa mastaa watano wa kikosi cha kwanza ambao wameiambia klabu wanataka kuhama dirisha hili la majira ya kiangazi.
Nyota huyo amekabidhiwa jezi hiyo ambayo iliwahi kuvaliwa na magwiji kwenye kikosi hicho.
Cunha, ambaye ni usajili wa kwanza wa Man United dirisha hili wakati saini yake iliponaswa kwa Pauni 62.5 milioni akitokea Wolves, alikuwa akiitolea macho jezi Namba 10 kabla ya kujiunga na miamba hiyo.
Cunha, 26, ambaye ni Mbrazili anaamini atarudisha makali ya Wayne Rooney kwenye klabu hiyo. Baadhi ya wachezaji mahiri kabisa wa Man United walivaa namba 10, hivyo kufanya jambo hilo kuwa na maana na presha kubwa kwa wachezaji.
Kwenye kikosi hicho Rashford amevaa namba tatu tofauti, 39, 19 na 10 - huku namba 10 alikabidhiwa 2018. Lakini, uamuzi wa kocha Ruben Amorim umebainisha kwamba baada ya ujio wa staa mpya Rashford hana nafasi tena.
Wachezaji wengine wanne walioomba kuondoka ni Alejandro Garnacho, Jadon Sancho, Antony na Tyrell Malacia. Amorim amewaambia wachezaji hao wakae mbali kwenye mazoezi yake ya pre-season waanze kufikiria hatima zao kwingineko.
Man United iliwaambia wachezaji hao idara ya utabibu itakuwa wazi kwao kama watahitaji kuitumia. Kama watashindwa kupata timu wiki chache zijazo, wataombwa kurudi Carrington baadaye. Rashford bado ana mkataba wa miaka mitatu, wakati Antony miwili na Sancho amebakiza mwaka.
Wachezaji wote hao walimalizia msimu uliopita kwenye klabu nyingine kwa mkopo.