Ten Hag afuta likizo Man United

Ten Hag afuta likizo Man United

MANCHESTER, ENGLAND. HII inaitwa hakuna kulala. Erik ten Hag ameripotiwa kuwataka mastaa wa Manchester United kuanza maandalizi ya msimu mpya mwishoni mwa Juni - ikiwa ni wiki mbili mapema zaidi kuliko ilivyokuwa imepangwa awali.

Mastaa wote wa Man United watahitaji mazoezini Juni 20, hiyo ina maana wachezaji hao watalazimika kukatisha mapumziko yao kwenye kipindi za majira ya kiangazi huko Ulaya.

Kocha Ten Hag anaamini kuwapa mazoezi ya ziada mastaa wake kutawapa uwezo wachezaji hao kuongeza kasi katika kucheza kwa staili yake ya kiuchezaji. Mdachi huyo anapenda soka la kushambulia na kukabia juu na baada ya kutazama mechi za Man United za karibuni ameona wachezaji wa Man United hawana uwezo huo.

Man United ratiba yao ya mechi za pre-season zimepangwa kuanza Julai 4, mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England. Lakini, ili kuwa na kikosi ambacho kitakuwa kwenye hali nzuri, Ten Hag ataomba wachezaji wake warudi mazoezini wiki mbili mapema zaidi. Ten Hag ameripotiwa kuwa na mpango wa kufanya mkutano kwa njia ya mtandao (zoom) na wachezaji wake ili kuweka wazi mipango yake kwa mastaa hao.

Kocha wa muda wa Man United, Ralf Rangnick amewahi kukosoa ufiti wa wachezaji hao baada ya kucheza hovyo zaidi kwenye mechi za Middlesbrough, Burnley na Aston Villa mapema mwaka huu.Kocha wa Southampton, Ralph Hassenhuttl naye aliwakosoa wachezaji wa Man United kwa kitendo chao cha kushindwa kupambana wanapokuwa hawana mpira katika mechi yao iliyomalizika kwa sare ya 1-1 uwanjani Old Trafford, Februari.

Kinachoelezwa, kocha Ten Hag amewaambia wanaohusika na mambo ya usajili kuhakikisha kutazama pia fursa ya kusajili wachezaji wanaopatikana bure kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, ambao bado wana ubora ili wawasajili.