Samatta mzigoni Uturuki

LIGI Kuu Uturuki inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo miwili kupigwa ukiwemo mchezo unaomhusisha nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa na chama lake la Fenerbahce dhidi ya BB Erzurumspor kwenye uwanja wa Kazim Karabekir.

Fenerbahce ambayo inaoenekana kuwa kwenye kiwango bora, itakuwa na kibarua kizigo leo cha kupigania pointi tatu dhidi ya BB Erzurumspor iliyo na mtiani ya kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja, jamaa wanaburuza mkia wakiwa na pointi 13.

Chama la Samatta linahitaji pointi tatu kwenye mchezo huo ili kuendelea kuweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo, wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 32 wamzidiwa pointi mbili na Besiktas wanaoongoza wakiwa na pointi 34. Msimamo huo ulikuwa kabla ya jana usiku, Besiktas kukabiliana na Hatayspor kwenye mchezo wa raundi ya 17 ambao wakina Samatta watacheza leo. Galatasaray wakiwa mchezo mmoja mbele wao ndio wapo nafasi ya pili wakiwa na pointi 33.

Tangu atoke majeruhi, Samatta amekuwa akitokea benchi ni mbinu ambazo zinaelezwa kuwa kocha wake,Erol Bulut amekuwa akitaka kumrejesha taratibu mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Tanzania kwenye kiwango chake.

Hadi sasa Samatta amecheza michezo miwili kwa dakika 16.