Ole amkataa Kane kisa anaye Anthony Martial

Monday October 28 2019
kane pic

MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer ametoa kali baada ya kusema Manchester United wala haimtaki Harry Kane kwa sababu tayari wanaye Anthony Martial.

Kocha huyo wa Man United amekuwa akiambiwa kwamba avunje benki kwenda kumsajili straika wa Tottenham, Kane aende akakipige Old Trafford ikiwa ni maneno ya gwiji wa mabingwa hao mara 20 wa England, Roy Keane.

Kocha Solskjaer anaamini Martial anaweza kuwa suluhisho la tatizo la ufungaji linalowakabili kwa sasa baada ya kuamua kumwondoa Romelu Lukaku kwenye kikosi na kumchukua jezi namba 9 kumkabidhi straika huyo Mfaransa, aliyenaswa kwa Pauni 45 milioni.

Martial aliifungia bao pekee Man United, Alhamisi iliyopita wakati walipoichapa Partizan Belgrade ugenini kwenye Europa League, lakini akiwa amerudi uwanjani siku za karibuni baada ya kuwa nje kwa wiki nane kutokana na kuwa na tatizo la maumivu ya misuli.

Na sasa kocha Solskjaer anaamini kwamba mshambuliaji wake namba moja amerudi, huku jana Jumapili walikuwa na shughuli ya kuwakabili Norwich City kwenye Ligi Kuu England.

“Sasa Anthony amerudi, nimefurahi sana kutokana na machaguo kuongezeka kwenye fowadi. Nimesikia watu wakisema kwamba tuna uhaba wa namba 9, lakini Anthony yupo na yupo vizuri ana kila kitu cha kuitendea haki nafasi hiyo,” alisema Solskjaer.

Advertisement

“Kwangu mimi, namwona Anthony ni namba 9 halisi. Anachohitaji ni kupata tu kasi ya mchezo, kwamba awe tu mchezoni muda wote. Nina hakika kama atakuwa anapata mipira na akiwa amejiweka kwenye nafasi sahihi, atakuwa anafunga mabao kama anavyotaka.”

Advertisement