Mane afunguka jambo Bayern

Mane afunguka jambo Bayern

MUNICH UJERUMANI.  SUPASTAA, Sadio Mane amefunguka na kudai kwamba kushuka kwa ubora wake ndani ya uwanja baada ya kutua Bayern Munich ni suala tu la kuzoea mazingira baada ya kuhama kutoka Liverpool kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi.

Mane alijiunga na Bayern Munich kwa mkwanja wa Pauni 35.1 milioni akitokea Liverpool, wakati alipoachana na klabu hiyo ya Anfield ambayo alibeba nayo mataji kibao kabla ya kuamua kwenda kukabiliana na changamoto mpya.

Mane alianza vizuri na miamba hiyo ya Bundesliga, alipofunga mabao manne katika mechi nne za kwanza, lakini baada ya hapo alicheza mechi tano bila ya kufunga, ikiwamo mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya na ile ya kichapo kutoka kwa Augsburg.

Mane alimaliza ukame wake wa mabao baada ya kufunga kwenye ushindi wa mabao manne dhidi ya Bayer Leverkusen, ambapo pia Bayern walimaliza ukame wao wa mechi nne za kucheza bila ya ushindi kwenye Bundesliga. Hivyo, ishu ya ubora ilikuwa ya timu nzima na si kwa Mane peke yake. Mane alifunga mabao 120 katika mechi 169 alizocheza Liverpool na kubeba mataji sita makubwa kwa muda wake aliokuwa chini ya kocha Jurgen Klopp, ambaye pia amekuwa kwenye wakati mgumu kwa kukosa huduma ya staa huyo.