Yanga yatanguliza wawili Nigeria

YANGA jana ilikuwa Uwanja wa Mkapa wakipambana na Wanigeria Rivers United, lakini kama ulidhani jamaa walikuwa na macho yote hapo unakosea na hesabu zao zilikuwa zinaangalia mchezo wa marudiano utakaopigwa wikiendi hii kule ugenini na kuna watu wameondoka leo haraka.

Yanga imewasafirisha watu wawili na mmoja kati ya hao kuna kigogo mzito anayejua kuchora ramani ya vita ambao wote wanakwenda kuchora ramani za jinsi gani timu yao itakavyoishi nchini humo.

Bilionea wa GSM, Ghalib Mohamed na kamati yake ya mashindano yenye vichwa tisa wamempa jukumu Kaimu Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa kutua haraka nchini Nigeria kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa.

Yanga tayari wana taarifa za kutosha kwamba Rivers wanaweza kuwaandalia mazingira magumu katika hatua za kuingia nchini humo lakini pia Senzo anatakiwa kwenda kuweka kila kitu juu ya hoteli na wapi watafanyia maandalizi yao ya mwisho kabla ya mchezo wa Septemba 19.

“Tuna rafiki zetu kule wamekuwa wakitupa mambo mbalimbali ya kule ambayo yametufanya tuanze hesabu hizo haraka na tunamwamini sana Senzo anajua mambo ya soka la Afrika, kwahiyo tumempa jukumu hilo la kutangulia,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati ya mashindano.

“Hatutaki kukwama sehemu ndio maana mnaona hatuangalii tu mchezo huu wa leo (jana) na Senzo ataondoka kesho (leo) Jumatatu) mapema kwenda huko Nigeria.

Mbali na Senzo pia ataambatana na mpishi maalum wa Yanga anayewaandalia chakula kule kambini kwao Avic Kigamboni anaenda kuungana na kiongozi wake kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kwenye misosi.

Mwanaspoti lina uhakika kwamba matajiri wa Yanga wameshakamilisha taratibu za kukodi ndege maalum ya Shirika la Tanzania litakaloipeleka timu hiyo siku mbili kabla ya mchezo na litabaki huko na kugeuza mara baada ya mchezo huo.