Yanga yakabidhiwa ubingwa kwa sare

Yanga yakabidhiwa ubingwa kwa sare

Muktasari:

  • Klabu ya Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya ikiwa muendelezo wa Ligi Kuu NBC

KLABU ya Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao la utangulizi kupitia kwa Heritier Makambo dakika ya 40, baada ya Hamadi Wazir 'Kuku' kushindwa kuuokoa mpira kabla ya Joseph Ssemujju kuisawazishia Mbeya City kwa penalti dakika ya 50 baada ya beki Bakari Mwamnyeto kuunawa mpira ndani ya eneo la 18.

Katika mchezo wa leo Mbeya City ilicheza pungufu baada ya beki wake Mpoki Mwakinyuke kupata kadi nyekundu dakika ya 44 kufuatia kumfanyia madhambi Juma Shaban na kusababisha timu yake kucheza wachezaji 10 uwanjani.

Hii ni sare ya pili msimu huu kwa timu hizi baada ya Februari 5, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kutoka suluhu ya 0-0.

Mchezo huu umetumika pia maalumu kwa ajili ya kuikabidhi Yanga ubingwa wa Ligi Kuu NBC baada ya kutangazwa rasmi Juni 15, ilipoichapa Coastal Union mabao 3-0 na kufikisha pointi 67 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Matokeo haya yanaifanya Yanga kufikisha pointi 71 ikiendelea kusalia kileleni huku ikisaliwa na mchezo wa mwisho Jumatano hii ya Juni 29, dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa upande wa Mbeya City imesogea hadi nafasi ya tisa na pointi 36 ikiendelea ikisalia na mchezo mmoja dhidi ya Namungo Juni 29 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema kuwa; "Tuna wachezaji wanaojua kumudu presha, mechi za msimu huu zilikuwa na presha kubwa sana. Tumepata sare lakini wachezaji wamefanya kila kitu kinachotakiwa kufanyika kwenye ligi, tutawahakikishia tutafanya vizuri hata fainali ya FA,".
Yanga wamebakiza mechi moja ya Ligi dhidi ya Mtibwa Sugar na moja ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Julai, 2 mwaka huu.