YANGA: TUONGEZE SAUTIII!

Monday September 28 2020
YANGA PIC

MASHABIKI wa Yanga jana walikuwa na furaha na kuwatania wenzao wa Simba wakiwauliza “wawaongezee sauti?” baada ya chama lao kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ambao waliwalazimisha Wekundu wa Msimbazi sare ya 1-1 wiki mbili zilizopita.

Kocha Zlatko Krmpotic ameendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote mpaka sasa tangu aanze kuinoa timu hiyo, baada ya jana vijana wake kumpa ushindi wa tatu mfululizo katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, huku akivunja mfupa uliowashinda watani wao.

Ndio, Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, ikiwa ni mara ya kwanza tangu zipite siku 1,824 waliposhinda mara ya mwisho dhidi ya Mtibwa katika uwanja huo.

Mara ya mwisho kwa Yanga kuifunga Mtibwa Jamhuri, ilikuwa Septemba 30, 2015 walipoitungua mabao 2-0 na baada ya hapo imekuwa ikipasuka ama kulamishwa sare kwa muda wa miaka minne, miezi 11 na siku 28 kabla ya jana beki Lamine Moro alipokata minyororo ya unyonge.

Lamine aliyekuwa nahodha wa mchezo huo alifunga bao hilo katika kipindi cha pili akiunganisha kwa mguu kona tamu ya Carlinhos aliyeanza kikosi cha kwanza jana na kuupiga mwingi, tofauti na wengi waliyodhani kutokana ubovu wa uwanja.

Hilo lilikuwa bao la pili kwa Lamine katika Ligi Kuu, likiwa pia linatokana na kona ya Carlinhos kwani hata kwenye mechi dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam alifunga kwa kichwa akiunganisha kona ya Muangola huyo na sasa wanaifanya Yanga ifikishe alama 10 na kulingana na watani wao watakaovaana nao Oktoba 18 katika Kariakoo Derby.

Advertisement

Carlinhos ameonekana akitumika kwa kazi maalum ya kupiga mipira iliyokufa na Muangola huyo alikuwa kwenye ubora kwani kona yake ya dakika ya 59 iliunganishwa na Lamine na kumfanya Kocha Zlatko kuzuia hata mabadiliko kwa dakika nne pale alipotaka kumtoa Carlinhos ili kumuingiza Yacouba Sogne.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Yanga walionekana mapema kuhitaji matokeo lakini hesabu za mashambulizi yao ndio kitu kilichowachelewesha huku pia hali ya uwanja ikichangia soka kutovutia.

Kipindi cha pili Mtibwa walirudi kwa kasi na kufanya shambulizi zuri dakika ya 56 mshambuliaji Ibrahim Ahmada alipoteza nafasi kwa kupaisha mpira akipokea pasi ya Salum Kihimbwa.

Lamine Moro aliwanyamazisha Morogoro kwa bao la dakika ya 59 akitumia kona ya Carlinhos, ambaye alikaribia kutoa asisti yake ya pili katika mechi ya jana kwa kona nyingine nzuri lakini Bakar Mwamnyeto alipiga kichwa cha ovyo huku kila mtu akidhani anafunga.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema walimuanzisha Carlinhos pembeni kwa kufahamu kuwa kutakuwa na faulo nyingi hivyo waitumie kwa mipira yake ya adhabu ndogo huku kocha wa Mtibwa, Zubery Katwila alisema yanga iliwazidi katika eneo la kati ambapo ilikuwa na viungo wengi.

MWADUI WAZINDUKA

Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Mwadui ilizinduka ikiwa nyumbani mjini Shinyanga kwa kuichapa Ihefu kwa mabao 2-0, huku Ruvu Shooting wakibanwa na Biashara United jijini Dar es Salaam kwa kutoka suluhu katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru.

Mabao ya Mwadui ambayo ni ya kwanza kwao tangu kuanza kwa msimu huu yaliwekwa kimiani na Fred Felix dakika ya sita likiwa bao la mapema zaidi mpaka sasa, kabla ya Wallace Kiango kuongeza la pili dakika ya 37.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya JKT Tanzania.

 

Advertisement