YANGA NI KAZE TENA

Monday October 05 2020
kaze pic

MWANASPOTI lilikuthibitishia ujio wa Kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic Yanga na jana lilikuwa la kwanza na pekee kufanya hivyo alivyofutwa kazi na waajiri wake.

Yanga ilimtema Zlatko usiku wa kuamkia juzi mara baada ya Yanga kumaliza mechi yao ya tano ya ligi ikishinda kwa mabao 3-0 dhid ya Coastal Union ukiwa ushindi wao mkubwa tangu ianze ligi msimu huu, lakini haukusaidia kunusuru ajira yake kwani tayari uongozi ulishafanya uamuzi kabla hawajaenda uwanjani.

Habari zinasema viongozi wa Yanga walimtema kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa timu pamoja na programu zake, huku wachezaji wakimlalamikia chinichini kwamba mazoezi yake laini kinoma, kiasi walihofia wasingeweza kuhimili mziki wa watani wao Simba watakaovaana nao Oktoba 18.

Lakini mpya za uhakika tena ni kwamba Yanga ina majina ya makocha watatu mezani, Cedric Kaze (Mrundi), George Lwandamina (Mzambia) na Roberto Oliveira Concalves do Carmo ‘Robetinho’ (Mbrazili).

Habari za uhakika Yanga imekubaliana kumuajiri Kaze ambae awali walishindwana nae kwani aliwaomba wampe wiki kadhaa aje nchini akitokea Canada ambako mkewe alikuwa akifanyiwa upasuaji.

Hersi Said, mmoja wa vigogo wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na Msimamizi wa Mdhamini GSM, aliliambia Mwanaspoti kwamba ; “Tupeni muda kidogo tumalize mchakato wa ndani ya klabu ila Kaze ni mmoja wao.”

Advertisement

Habari zinasema, Hersi amekuwa na mazungumzo ya kina na Kaze na wamekubaliana mambo kadhaa ingawa anaonekana kuingiwa hofu kutokana na Zlatko kutimuliwa ndani ya mwezi mmoja.

Habari zinasema Kaze amewaambia Yanga wampe wiki tatu akamilishe mambo yake na kujiunga nao, huku muda huo msaidizi wake Juma Mwambusi akiendelea na mzigo.

Kaze ambaye amehusika kwenye usajili wa sasa wa Yanga pamoja na kuwajua wachezaji hao hususani Michael Sarpong, Tuisila Kisinda, Haruna Niyonzima na Mukoko Tonombe, atakuwa jukwaani kwenye mechi ya watani huku Mwambusi na Said Maulid wakilisongesha.

“Kaze atakuja mambo mengi yameshawekwa sana, ameshawishika, ingawa kuna wajumbe kwenye Kamati ya Utendaji wanataka arudishwe, Lwandamina ambaye amewahi kuwa ndani ya Yanga na anaujua utamaduni wetu. Lakini mpaka sasa uwezekano mkubwa ni Kaze, ndiye Kocha wetu,” alidokeza kigogo mmoja wa Yanga mwenye ushawishi na anayehusika kwenye uamuzi wa mambo mengi Jangwani.

Alidokeza pia, Hersi alishakutana na Robertinho mara kadhaa wakajadiliana, lakini bado hakushawishika kama ilivyo kwa Kaze ambaye ikitokea imeshindikana tena dakika za mwisho atatua Lwandamina ambaye ameachana na Zesco United wiki chache zilizopita kabla haijamsajili David Molinga ‘Falcao’ aliyetemwa na Yanga.

Jana Mshauri wa Uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa aliposti kwenye Tweeter yake kwamba wanaamini uamuzi waliofanya ni sahihi na watatumia muda huu wa mapumziko wa mechi ya Taifa Stars na Burundi kujipanga upya na kila kitu kitakwenda sawa.

Advertisement