Watakula nyingiiii!

YANGA leo imepanga kufunga busta kubwa kwenye mechi yake ya Kombe la FA dhidi ya Kengold FC. Kwenye kikosi cha kwanza kitakuwa na sura tatu mpya ambazo ni Carlos Carlinhos, Yacouba Sogne na Fiston Abdul Razak.

Kocha wa Yanga amepanga kumuanzisha Carlinhos na Yacouba ambao walikuwa majeruhi kwa kipindi kirefu, ingawa Carlinhos alipewa dakika kadhaa kwenye mechi na Mtibwa Sugar akaingia kufunga bao la ushindi. Kwa mujibu wa mazoezi kikosi kitakachoanza leo saa 10 huenda kikawa hivi; Shikhalo, Boxer, Adeyun, Ninja, Moro, Dickson, Nchimbi, Kaseke, Waziri, Fiston na Carlinhos.

Baada ya Simba kutamba kwa wiki nzima, mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz alitamba jana kwamba ; “kuna mtu anakula nyingi.” Akimaanisha mpinzani wao Kengold FC ya ya Mbeya leo katika Uwanja wa Uhuru jijini ukiwa ni mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho la Azam linaloamua timu ya kucheza michuano ya Shirikisho Afrika msimu ujao. Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa raundi ya nne ya mashindano hayo tangu yalipoanzishwa msimu wa 2015/2016.

Timu hizo hazijawahi kukutana hata katika mchezo wa kirafiki na hii itakuwa mara ya kwanza kwao kucheza katika mechi inayoonekana itatawaliwa zaidi na Yanga licha ya Kengold kutamba kwamba wanaelewa udhaifu wa Yanga na watawashangaza. Ratiba ngumu ambayo iko mbele ya Yanga mara baada ya kuivaa Kengold italazimisha benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Cedrick Kaze kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ingawa amesisitiza mechi hiyo ni muhimu na hataidharau.

“Haya ni mashindano na hatupaswi kudharau timu yoyote tunayokutana nayo hivyo kwetu sisi hii ni mechi ambayo hatuwezi kuidharau na tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri tuweze kusonga mbele,” alisema Kaze ambaye ni raia wa Burundi. Licha ya kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 49,

Ushindani inaoupata kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu kutoka kwa Simba, unailazimisha Yanga kuhakikisha inafanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho la Azam kwani bado haijawa na uhakika mkubwa kwamba itatwaa taji la Ligi Kuu ambalo litaiwezesha kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga na Kengold zinakutana katika mchezo huo kila moja ikiwa na hali nzuri kisaikolojia kutokana na nafasi iliyopo katika ligi ambayo inashiriki.

Wenyeji Yanga ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini Kengold yenyewe inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi A la Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na pointi 16 ambazo imekusanya katika jumla ya mechi 10 ilizocheza hadi sasa.

Kengold inaweza kunufaika na kutofahamika kwake na Yanga kuweza kuwasumbua mabingwa hao mara moja wa taji hilo jambo ambalo hata Kaze amekiri; “Hatuwafahamu vizuri wapinzani wetu hivyo tunatakiwa kuwa na umakini na tahadhari ya hali ya juu dhidi yao,” alisema Kaze.

Baada ya kuivaa Kengold ambayo awali ilifahamika kama Geita Gold, Yanga itakuwa na mechi mbili ngumu ugenini za Ligi Kuu ndani ya muda wa saa 72 ambapo mchezo wa kwanza utakuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga watakapowafuata Coastal Union katika mechi itakayopigwa Machi 4 na siku tatu baadaye itasafiri hadi Moshi kuumana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika.

Kabla ya mechi hiyo ya Yanga, Maafande wa Polisi Tanzania wataanza kwa kuikaribisha Kwamndolwa FC katika uwanja wa Ushiriki, Moshi, mechi ambayo itachezwa kuanzia saa 8.00 mchana na saa 1.00 usiku, Azam FC watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex kucheza na Mbuni FC.


WASIKIE KEN GOLD

Naye kocha wa timu hiyo, Salvatory Edward ‘Dokta’ alisema mbali na kusaka ushindi, lakini inaweza kuwa na neema kwa wachezaji wake kutoka, kwani wanaweza kujiweka sokoni.

Edward aliyewahi kutamba na Yanga na Taifa Stars akiwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa na miili mikubwa na waliokuwa wakiheshimika zaidi na mashabiki wa Jangwani, alisema watawakabili wapinzani wao kwa heshima kutokana na historia kubwa waliyonayo lakini hesabu kubwa ikiwa ni kushinda mchezo huo na kufuzu hatua inayofuata.

“Inawezekana wachezaji wangu ikawa mara ya kwanza kukutana na Yanga, lazima tuwaheshimu lakini kutumia nafasi hiyo vijana kujitangaza na kutoka kimpira. Kikosi changu kimekamilika sina majeruhi yeyote wala mwenye sababu ya kukosa mchezo huo, tumejipanga kwenda kupamabana na ikiwezekana hii michuano tubebe ubingwa” alitamba kocha huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa zamani wanaoanza kuchipukia kwenye ukocha akiamua kuanzia ngazi ya chini ili aimarike zaidi kiufundi.