Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wamemfuata Lowassa

Said Bahanuzi

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa amelikimbia benchi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Licha ya kukaa katika chama hicho kwa miaka mingi bado alishindwa kupata tiketi ya kugombea Urais hivyo kuamua kuhamia Chadema ambayo ilikubali kumpa ridhaa hiyo.

Baada ya kuhama tu, baadhi ya wanachama wa CCM waliokuwa benchi nao wameamua kumfuata taratibu. Wameenda kupandisha viwango vyao katika vyama vya upinzani ili baadaye waweze kuwa viongozi wakubwa tena. Ni mapinduzi ya kipekee katika siasa.

Wakati hayo  ya Lowassa na wengine kutimkia upinzani yakivuma, wapo wachezaji kadhaa nao wameona ni vyema wakachukua uamuzi kama wa Lowassa.

Nyota hawa waliokuwa wakisugua benchi katika klabu zao za zamani na wamejiunga na klabu nyingine za Ligi Kuu ili kwenda kupandisha viwango vyao.

Mwanaspoti inakuletea baadhi ya wasugua benchi walioamua kufuata nyayo za Lowassa na wanasiasa wengine waliokimbilia katika kambi ya upinzani.

Hussein Javu

Straika, Hussein Javu ameshtuka kitu pale Yanga na kuamua kurejea katika klabu yake ya zamani ya Mtibwa Sugar. Javu ni aina ya wachezaji wazuri na wapambanaji lakini kwa bahati mbaya Yanga haikumkubali. Msimu uliopita alicheza mechi zisizozidi nne na muda mwingi alikuwa anasugua benchi. Ujio wa Donald Ngoma na Malimi Busungu ndiyo umeonekana kuwa sumu zaidi kwa Javu hivyo kuamua kutimka.

Rajab Zahir

Beki wa kati, Rajab Zahir ameshindwa kuwapa changamoto mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani pale Yanga kwa muda, hivyo kuamua kwenda kwa mkopo Stand United ya Shinyanga ili kuimarisha kiwango chake.

Licha ya kuwepo pale Yanga kwa misimu miwili iliyopita, bado Zahiri alishindwa kuonyesha cheche za maana na kuishia kusugua benchi kwa muda mwingi. Mechi alizocheza msimu uliopita ni chache kuliko umri wa mtoto anayetakiwa kujiunga na darasa la kwanza.

Hussein Sharif

Kipa huyo maarufu kama Casillas alijiunga na Simba msimu uliopita, lakini hakubahatika kuwa na maisha mazuri klabuni hapo. Aliumia mara baada ya mechi tatu tu za ligi na kulazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Hata hivyo, licha ya kurejea uwanjani mwishoni mwa Januari, Casillas alishindwa hata kuwa chaguo la pili katika kikosi hicho cha Simba hadi msimu ulipomalizika mwezi Mei.

Kipa huyo bora wa msimu wa 2013/14 ameamua kufuata nyayo za Lowassa baada ya kujiunga na Mtibwa Sugar aliyokuwa akiichezea hapo awali.

Said Bahanuzi

Straika, Said Bahanuzi alikuja mjini na kufanya yake mapema mwaka 2012, lakini baada ya hapo maisha yalibadilika na kuwa magumu kwake. Akitokea kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012 straika huyo hakufanikiwa kufikisha idadi ya mabao 10 kwa msimu hata mmoja katika kipindi cha miaka yake mitatu pale Yanga.

Kutokana na hali hiyo, Bahanuzi ameamua kurejea katika kikosi cha Mtibwa Sugar ili kupandisha kiwango chake. Maisha ya benchi pale Yanga yangemmaliza kabisa.

William Lucian ‘Gallas’

Kiraka, William Lucian ‘Gallas’ alikuwa na nafasi kubwa ya kupewa mkataba pale Simba, ila nafasi ya kucheza ndiyo ilikuwa tatizo. Unafikiri angecheza wapi pale Simba. Kule beki ya kulia yupo Hassan Kessy ambaye katika mabeki watatu bora wa kulia nchini hakosekani. Katika nafasi ya kiungo wapo Justice Majabvi, Jonas Mkude, Awadhi Juma na Abdi Banda ambao bila shaka wako katika ubora wa juu kwa sasa.

Hapa hakukuwa na namna kwa Gallas, hivyo kuamua kuchukua uamuzi kama wa Lowassa na kutimkia Ndanda ya Mtwara.

Abdallah Seseme

Kiungo, Abdallah Seseme alitamba na Simba vilivyo msimu wa 2012/13, lakini baadaye alipata majeraha ambayo yalisababisha apate nafasi ya kudumu katika benchi la timu hiyo. Seseme alipopona alikuta Said Ndemla na viungo wengine wakiwa katika ubora wao, hivyo kukosa nafasi ya kucheza pale Simba. Licha ya mkataba wake kumalizika, Seseme bado alihitajika kufanya uamuzi kama wa Lowassa ili kupandisha kiwango chake. Kwa sasa kiungo huyo amejiunga na Toto Africans ya Mwanza ambayo bila shaka itampa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Amri Kiemba

Kiungo, Amri Kiemba alipelekwa kwa mkopo na Simba pale Azam mwishoni mwa mwaka jana, lakini maisha ya benchi aliyokutana nayo yalimsababisha afanye uamuzi mgumu kama Lowassa.

Kiemba hakucheza mechi zaidi ya tano pale Chamazi hali ambayo ilihatarisha kiwango chake.

 Kiemba amejiunga na Stand United ya Shinyanga ili kupata nafasi ya kucheza msimu huu. Kwa hali ilivyokuwa pale Azam uamuzi wake unaonekana kuwa wa busara zaidi.