Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wagombea 25 wajitosa uchaguzi TFF

WAGOMBEA Pict

Muktasari:

  • Uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za uongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa TFF, umefungwa jana Ijumaa jioni.

BAADA ya uchukuaji na urudishaji wa fomu kutamatika jana Juni 20, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kiomoni Kibamba amesema wagombea sita wa urais wamezirudisha, huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji ikiwa ni 19.

Uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za uongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa TFF, umefungwa jana Ijumaa jioni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kibamba amesema zoezi lilifungwa jana na wagombea waliochukua na kurudisha fomu kwa upande wa wagombea urais ni sita na kwa upande wa kamati ya utendaji ni 19, hivyo jumla kuwa 25

"Sipo kwenye nafasi nzuri ya kukutajia majina yote kwa nafasi hizo, sifahamu bado, lakini idadi ndio hiyo niliyokutajia," amesema.

Mwanaspoti linafahamu waliochukua fomu kwa upande wa nafasi ya rais kuwa ni Ally Mayay na Shija Richard, Dk Mshindo Msolla na Wallace Karia anayetetea kiti, lakini miongoni mwa wagombea hao wamelia kukosa wadhamini wanaotakiwa kuwaidhinisha ili kukidhi kanuni za uchaguzi wa TFF za mwaka 2021 zinazotaka wapate wajumbe wa Mkutano Mkuu si chini ya  watano.

Katika uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 16 jijini Tanga, nafasi saba zinawaniwa ikiwamo moja ya urais na sita za wajumbe wa Kamati ya Utendaji, na jana ilikuwa mwisho wa kurudisha fomu baada ya uchukuliwaji wa fomu hizo kuanza tangu Jumatatu (Juni 16).

Kanuni ya Uchaguzi ya Mwaka 2021 Ibara ya 10 (3 -4) inaeleza kuwa mgombea wa urais wa TFF lazima awe na barua tano za udhamini kutoka kwa wanachama wa TFF, huku kwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka kanda lazima awe na barua ya udhamini kutoka chama cha soka cha mkoa husika.

Inaongeza kuwa, mwanachama hapaswi kumdhamini mgombea zaidi ya mmoja kwa nafasi moja vinginevyo udhamini wote utakuwa batili.

Kwa mujibu wa orodha hiyo wanaotoa uidhinishaji kwa wagombea ni 47 ambao mchanganuo wake upo hivi vyama vya soka vya mikoa (FA) vyenye wajumbe 26, klabu za Ligi Kuu Bara (16) huku Chama wa Waamuzi Tanzania (FRAT), Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TSMA), Chama cha Wachezaji (SPUTANZA) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) kila kimoja kikiwa na mjumbe mmoja.