Waarabu wamefika bei kwa Miquissone

BAO kali la Luis Jose dhidi ya Al Ahly limewapandisha mzuka Waarabu na wameanza kufika bei kwa kupiga simu na kutumatuma vimeseji kwenye WhatsApp wakiulizia kama jamaa anapatikana.

Iko hivi, kabla ya mechi ya juzi, klabu tatu tofauti ikiwemo haohao Al Ahly zilikuwa zikimtolea udenda Miquissone baada ya kukoshwa na uwezo wake, lakini bao alilofunga juzi, limeongeza tamaa zaidi kwa timu hizo ambazo tayari zimeanza harakati za kumnasa.

Mwanaspoti limejulishwa kuwa tayari kuna ofa tatu mezani kwa Simba kutoka kwa klabu kubwa Afrika zikimhitaji nyota huyo na kilichobaki ni uongozi wa timu hiyo na Luis mwenyewe kuamua wapi aelekee msimu ujao. Lakini wakubwa wa Simba hatahivyo hawako tayari kumuuza kwa sasa. Kati ya ofa hizo tatu, mojawapo inatoka Al Ahly na nyingine ni ya CR Belouzdad ya Algeria ambayo iko hapa nchini kucheza mechi yake ya Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini Jumapili ijayo, ingawa ofa ya tatu bado haijatajwa inatoka klabu ipi hasa ingawa inatajwa kuwa ni kubwa Afrika

“Kuna viongozi wa Belouzdad walikuja kutazama mechi na wameonekana kuvutiwa na Miquissone na wametuuliza kuhusa mkataba na thamani yake hivyo wameahidi watatuletea ofa rasmi,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Kutokana na hilo staili ya ufungaji pamoja na thamani ya idadi ya nyota tisa wa Al Ahly walioshindwa kumdhibiti Miquissone wakati akiifungia Simba bao pekee la ushindi juzi inaweza kuleta neema kwa winga huyo na klabu yake siku za usoni.

Nyota huyo wa Simba alitumia uwezo binafsi kuwazidi ujanja wachezaji tisa wa Al Ahly na kuifungia Simba, bao lililoifanya ikae kileleni mwa msimamo wa kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu baada ya kufikisha pointi sita katika mechi mbili.

Miquissone alifunga bao hilo katika dakika ya 31 ya mchezo kwa shuti kali la mguu wa kulia lililomshinda kipa Mohamed El Shenawy wa Al Ahly na kujaa kimiani mara baada ya kupokea pasi fupi kutoka kwa Clatous Chama.

Mara baada ya kupokea pasi hiyo ya Chama, Miquissone aliwahadaa wachezaji wazuri wa Al Ahly, Aliou Dieng na Akram Tawfik na kisha kuacha fataki ambalo lilikwenda kutikisa nyavu za wapinzani wao.

Lakini ukiachana na ufundi uliotumika katika kufunga bao hilo, Miquissone aliwazidi ujanja wachezaji tisa wa Al Ahly ambao waliwepo jirani naye wakati anapokea pasi hiyo ya Chama na kuujaza mpira wavuni.

Jambo la kushangaza zaidi, wachezaji hao tisa walioshindwa kumdhibiti Miquissone asifunge bao hilo, kwa jumla wana thamani ya zaidi ya Sh 27.2 bilioni ambayo inazidi hata thamani ya uwekezaji ya klabu ya Simba.

Wachezaji tisa ambao walizidiwa ujanja na Miquissone wakati anafunga bao hilo ni kipa Mohamed El Shenawy, mabeki Mohamed Hany, Mahmoud Wahid, Badr Banoun na Yasser Ibrahim, viungo Hamdi Fathi, Akram Tawfik na Aliou Dieng pamoja na mshambuliaji Junior Ajayi ambao kwa mujibu wa mtandao wa uhamisho wa wachezaji hao wana thamani ya Euro 9.8 milioni (Sh 27.2 bilioni).

Wakati Miquissone anafunga bao hilo, golini alikuwepo mchezaji ghali zaidi katika kikosi cha Al Ahly, kipa na nahodha El Shenawy ambaye thamani yake ni Euro 2.5 milioni (zaidi ya Sh 6.9 bilioni).

Mbele karibu kabisa na Miquissone, alikuwepo kiungo raia wa Mali, Aliou Dieng ambaye kwa sasa thamani yake sokoni ni Euro 1.5 milioni (Sh 4.2Bilioni) ambaye kushoto kwake alikuwepo kiungo Akram Tawfiq mwenye thamani ya Euro 400,000 (zaidi ya Sh 1.1 bilioni). Jirani nao upande wa kulia, kulikuwa na beki wa kulia wa Al Ahly, Mohamed Hany mwenye thamani ya Euro 1 milioni (Sh 2.7 bilioni), na nyuma yao walikuwepo mabeki wawili wa kati, Badr Banoun na Yasser Ibrahim. Thamani ya Badr Banoun ni Euro 1.1 milioni (Sh 3.1 bilioni) huku ile ya Yasser Ibrahim ikiwa ni Euro 600,000 (Sh 1.7 bilioni). Ukiondoa hao, kulikuwepo pia kiungo Hamdi Fathi mwenye thamani ya Euro 800,000 (Sh 2.2 bilioni), beki wa kushoto Mahmoud Wahid mwenye thamani ya Euro 400,000 (Sh 1.1 bilioni) ambaye mbele yake alikuwepo mshambuliaji Junior Ajayi mwenye thamani ya Euro 1.5 milioni (Sh 4.2 bilioni) ambaye alishuka chini kusaidia ulinzi.

Lakini wakati nyota hao tisa wa Al Ahly wakiwa na jumla ya thamani hiyo ya fedha, Miquissone aliyefunga, ana thamani ya Euro 150,000 (Sh 416 milioni) kwa mujibu wa mtandao huo wa www.transfermarkt.com.