VPL SPESHO: Ghafla upepo umebadilika

Muktasari:

NI wanasoka wakali ila walichofanya msimu huu wa Ligi Kuu wamestaajabisha na kuwaachia mashabiki swali ambao walijawa na matumaini makubwa kutoka kwenye miguu yao.

NI wanasoka wakali ila walichofanya msimu huu wa Ligi Kuu wamestaajabisha na kuwaachia mashabiki swali ambao walijawa na matumaini makubwa kutoka kwenye miguu yao.

Ligi hiyo inamalizika jana Jumapili, huku Simba tayari imetangaza ubingwa mara ya nne mfululizo. Mwanaspoti linakuchambulia baadhi ya wakali waliostaajabisha mashabiki kutokana na kazi ya miguu yao iliyowaachia mshangao.


MICHAEL SARPONG -YANGA

Yanga ilimsajili straika wa mabao Sarpong akitokea Rayon Sports ya Rwanda na alikabidhiwa jezi namba 19, wakitarajia makubwa kutoka kwake. Lakini ni kama ameishia kuwachefua mashabiki kwani katika mabao 50 ya timu amechangia manne sawa na beki Lamine Moro.


MEDDIE KAGERE-SIMBA

Ndani ya misimu miwili mfululizo straika wa Simba, Meddie Kagere ndiye alinyakua kiatu cha dhahabu 2018/19 akiwa na mabao 23 na 2019/20 mabao 22. Ana mabao 13 kabla ya mechi ya mwisho ya leo na hajawapa raha mashabiki kama ilivyotarajiwa.

Misimu miwili nyuma alikuwa anawaka, anazungumzwa kila sehemu akishangilia kwa mbwembwe na kufunga mabao. Ligi hii ni kama imemkataa na amekuwa wa kawaida kabisa.


BENARD MORRISON - SIMBA

Winga wa Simba mwenye vituko vyake, Morrison, Mei 29, Uwanja wa Majaliwa alifanya kitu cha kustaajabisha baada ya kufunga bao mojawapo kati ya 3-1 dhidi ya Namungo FC la umbali mrefu, ambalo lilijadiliwa zaidi katika mitandao ya kijamii na huenda likaingia kwenye rekodi bora.

Ukiachana na bao hilo, jambo lingine lililostaajabisha kwa Morrison ni matarajio ya mashabiki wa Simba kumtarajia kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa Yanga ambako alikuwa anatisha kwa kufanya maajabu uwanjani.


HARUNA NIYONZIMA-YANGA

Ni mwaka wa 10, Niyonzima kucheza soka la Bongo. Mara ya kwanza alijiunga na Yanga msimu wa 2011 -2017, kisha akahamia Simba 2017-19 ambako hakuwa na msimu mzuri na 2019 alijunga na A.S Kigali ya Rwanda. Yanga ilimrejesha tena Niyonzima 2020/2021 baada ya kumuona anafanya vyema A.S Kigali. Ajabu baada ya kujiunga nao hakuna maajabu aliyoyaonyesha, jambo ambalo limewaachia swali mashabiki kutaka kujua amepatwa na jambo gani mguuni kwake kushindwa kutema madini. Hata hivyo kiungo huyo ameagwa Yanga.


PERFECT CHIKWENDE - SIMBA

Simba ilimsajili straika Perfect Chikwende baada ya kuwasumbua katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na FC Platinum ya Zimbabwe. Ujio wake ndani ya kikosi hicho ulibeba matarajio kuongeza thamani kubwa ya safu ya mbele ya timu.

Ajabu alichokionyesha Chikwende kimewastaajabisha mashabiki na amewakata stimu ya kumshobokea. Amefunga bao moja tu mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya African Lyon.


MPIANA MONZINZI - AZAM FC

Usajili wa straika wa Azam FC, Monzinzi kutoka FC Lupopo ya DR Congo ulikuwa mzito na mashabiki walitarajia angewapa kazi ngumu mabeki kumkaba. Ajabu amekuwa mchezaji wa kawaida na hana ushindani mbele ya wazawa.


ALLY NIYONZIMA- AZAM FC

Alitua nchini kufanya mazungumzo na Yanga waliompotezea. Baadaye alijiunga Azam FC msimu wa 2019-2021 akitokea Rayon Sports ya Rwanda. Wakati huo jina lake lilikuwa na nguvu kutokana na kiwango alichokionyesha akiwa kwao. Ajabu kwa sasa ni wa kawaida.


OBREY CHIRWA - AZAM FC

Kiwango cha Chirwa wakati yupo Yanga alikuwa tishio kwa mabeki. Alipojiunga Azam FC alionyesha uwezo mkubwa mwanzoni baadae amekuwa wa kawaida kabisa - makali yake yamepungua.


AME ALLY- SIMBA

Alikuwa kikosi cha kwanza Coastal Union ya Tanga. Baada ya kutua Simba nafasi yake imekuwa finyu mbele ya kocha wa timu hiyo, Didier Gomes. Amekuwa akiingia kipindi cha pili mara mojamoja.


FISTON ABDULRAZAQ - YANGA

Mashabiki wa Yanga walifurahia usajili wa Fiston waliyemtoa NPPI ya Misri. Walikuwa na matarajio ya angesaidiana na Saido Ntibanzokiza kwamba wangefanya maajabu. Ajabu yake amekuwa mchezaji wa kawaida anayewachefua mashabiki kwa kushindwa kucheka na nyavu kama walivyomtarajia.


SAIDO -YANGA

Miongoni mwa wachezaji waliopata kibali cha kupendwa na mashabiki wa Yanga ni straika Saido ambaye walimsajili msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi. Ana akili kubwa ya kazi ingawa inakinzana na mwili kutokana na umri kumtupa mkono. Saido anayemiliki mabao manne ana nyota kali kila anapofunga kwanihuzungumziwa kila kona. Lakini hadi ligi inamalizika amepoa.


BENO KAKOLANYA - SIMBA

Tangu Kakolanya alipojiunga na Simba akitokea Yanga licha ya kuonyesha uwezo pindi anapopata nafasi finyu mbele ya mshindani wake, Aishi Manula, anaonekana wa kawaida sana na kustaajabisha wengi ambao walimuona akiwa kwenye kiwango bora enzi zake Yanga.


PETER MAPUNDA - DODOMA JIJI

Wakati anasajiliwa na Dodoma Jiji msimu huu, Mapunda alitarajiwa kuisaidia timu kufunga mabao mengi kutokana na kuvutiwa na huduma yake akiwa na Mbeya City ambako alimaliza msimu na mabao 13, ila hadi sasa ligi anamiliki bao moja.