Viungo Simba wamaliza ishu

Wednesday October 14 2020
viungo simba pic

CAF imeonyesha majina ya klabu nane kutoka Arabuni zilizofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu huku staa wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amesema uimara wa viungo utawabeba na kuwakomesha Waarabu msimu huu.

Lakini, akaongeza kuwa wanahitaji kuongeza mbinu tu kabla michuano hiyo haijaanza Novemba 27 huku ratiba ikipangwa wiki ijayo.

Alifafanua kuwa Simba ina viungo wengi wazuri ambao ni Benard Morrison, Clatous Chama na Luis Miquissone huku akisema tatizo lao timu isipokuwa na mpira hawawezi kukaba kuurudisha kwenye himaya yao, hivyo wanakuwa na wakati mgumu wakutoonekana wanafanya nini uwanjani.

“Soka la sasa linamtathimini mchezaji asipokuwa na mpira anaweza akaurejeshaje kwa timu yake, hicho kitu kwao ni tatizo, ingawa kwa kuchezesha timu ni mafundi na wataisaidia kwenye michuano hiyo, sasa jukumu la kukaba linakuwa kwa wachache ambao ni Jonas Mkude na Mzamiru Yasin,” alisema Pawasa.

“Safu ya mabeki inatakiwa kuongezewa nguvu kutokana na soka la nchi hizo kuwa juu, haijalishi watapangwa na timu kutoka Algeria, Congo, Misri, Morocco ama Tunisia, wana washambuliaji wenye utashi wa juu, hivyo kocha afanye kazi ya kuiweka imara, ikiwemo kipa Manula ili mabeki wakipoteana awe anainusuru timu,” alisema beki huyo aliyecheza Simba kwa mafanikio.

Ukiachana na maneno ya kiungo na ulinzi aliyoyafafanua kiundani, alisema timu itatakiwa kucheza kwa nidhamu akitolea mfano wa Shomary Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuwa wananyumbulika katika majukumu yao ikiwemo kusaidia kushambulia, jambo alilowataka wawe na umakini kurudi kwa haraka.

Advertisement

“Sio vibaya kuisaidia kushambulia, ila kwa kocha mjanja anapoona mabeki wote wa pembeni wako kwake basi mashambulizi ya kushtukiza ni hatari sana,” alisema Pawasa.

Kuhusu eneo la ushambuliaji, Pawasa alisema kuna wapambanaji wazuri na jambo la kurekebisha ni kucheza kwa kuzoeana.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema eneo la ulinzi la kati ambalo wanasimama Pascal Wawa na Joash Onyango linatakiwa marekebisho kwani, hawana kasi hivyo wanaweza kuigharimu timu kimataifa.

“Kocha awasaidie Wawa na Onyango kucheza kwa kasi, washambuliaji wa timu hizo, soka lao lipo juu hivyo ni rahisi kupinduliwa pinduliwa, lakini maeneo mengine wapo vizuri na wanaweza wakaonyesha ushindani,” alisema Baraza.

Baraza aliangazia eneo lingine la nidhamu ya wachezaji wa Tanzania kuwa chini, aliwataka waepuke kuwafokea waamuzi kama wanavyofanya kwenye ligi ya ndani, jambo alilosema wachezaji wa klabu za Magharibu wanalitumia kama mbinu kumaliza wapinzani.

“Waamuzi wa kimataifa ni tofauti na hawa wa Tanzania, wale kosa moja ni adhabu, udhaifu huo wanautumia sana Waarabu kuwaadhibu wapinzani,” alisema.

WAARABU 8 HAWA

Kwa mujibu wa vigogo wa ndani ya CAF ni kuwa ratiba itatoka baada ya nusu fainali za Ligi ya Mabingwa na Shirikisho za wikiendi hii.

Kwa mujibu wa orodha mpya iliyotolewa na Caf, kuna timu nane kutoka Morocco kuna Raja Casablanca na Wyadad Casablanca, Misri kuna Al Ahly na Zamalek wenye asilimia kubwa ya kuwa wa pili.

Esperance de Tunis na CS Sfaxien zitaiwakilisha Tunisia, Algeria ni CR Belouizdad na MC Alger. Licha ya wawakilishi kutoka kanda zingine lakini maranyingi timu za nchi hizo nne ndizo zimekuwa hofu ya klabu za Afrika Mashariki. DR Congo itakuwa na TP Mazembe na AS Vita. Simba tayari imefanya ziara nzito Misri kuangalia Ahly na Zamalek wanafanya nini katika uendeshaji na kujifunza kitu.

Advertisement