Vituko kambi ya Simba

Kocha wa timu ya Simba Dylan Kerr
Muktasari:
Timu inafanya mazoezi kati ya saa nne hadi tano kwa siku. Kutokana na hali ya hewa ya baridi wachezaji wanaonekana kuyafurahia mazoezi na kufanya bila kutegea, hivyo kupunguza usimamizi wa kocha huyo.
KAMBI ya Simba mjini hapa inakwenda vizuri, wachezaji wanaonekana kuimarika vilivyo. Kocha mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr anaonekana kuwa mwingi wa furaha kutokana na matokeo chanya ya kambi hii.
Timu inafanya mazoezi kati ya saa nne hadi tano kwa siku. Kutokana na hali ya hewa ya baridi wachezaji wanaonekana kuyafurahia mazoezi na kufanya bila kutegea, hivyo kupunguza usimamizi wa kocha huyo.
Mbali na mafanikio hayo yaliyoanza kujionyesha, kuna baadhi ya upungufu ulioonekana mpaka sasa. Mwanaspoti linakuletea baadhi ya upungufu na vituko vilivyotokea hapa Lushoto mpaka sasa.
Hakuna kiongozi
Katika hali ya kushangaza kwa wiki nzima ambayo Simba imekuwa mjini hapa, hakuna kiongozi yeyote wa timu hiyo aliyekuwepo. Timu iko chini ya Kocha Kerr na msaidizi wake, Selemani Matola. Si rais wa timu hiyo, Evans Aveva, makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ama Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mohammed Nassoro aliyefika hapa. Kaimu katibu wa timu hiyo, Colins Frisch aliwasili hapa juzi Jumamosi jioni ikiwa ni wiki moja tangu ilipoanza mazoezi.
Matola na Kerr walilazimika kufanya kila kitu hapa ikiwemo masuala ya kiutawala. Sidhani kama ni sahihi kwa kocha kuhangaikia suala la usafiri wa timu kwenda mazoezini. Sidhani kama ni sahihi kwa kocha kuhangaika kutafuta hoteli ya kuhamia ili kuisogeza timu karibu na uwanja wa mazoezi. Haya ni masuala ya kiutawala lakini kwa kuwa hakukuwa na kiongozi hapa, yanalazimika kufanywa na Kerr na Matola.
Kumbe DC hajui
Katika hali ya kushangaza, kumbe Simba imeweka kambi hapa Lushoto bila kutoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya (DC) wa hapa, Mariam Juma wala Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD). Mkuu huyo wa wilaya alisema licha ya kwamba Tanzania ni nchi huru, ni jambo la busara kwa timu kubwa kama Simba kutoa taarifa kwa viongozi wa wilaya kwa sababu za kiusalama. Mariam alisema endapo timu hiyo itapata tatizo lolote la kiusalama mjini hapa, lawama zinaweza kwenda kwao wakati wao hawana taarifa zozote mpaka sasa.
Hata hivyo, licha ya kutopewa taarifa yoyote, mkuu huyo wa wilaya alitoa ahadi ya kutembelea kambi ya timu hiyo, jana Jumapili jioni.
Hakuna jezi za mauzo
Simba ina mashabiki hapa Lushoto usiambiwe na mtu, ni wengi kweli kweli, lakini katika hali ya kushangaza timu hiyo haikubeba hata jezi moja kwa ajili ya kuziuza kwa mashabiki wake wa hapa. Mashabiki hao kila siku wamekuwa wakiulizia sehemu wanayoweza kupata jezi hizo lakini hakuna majibu yanayoeleweka.
Wakati huu ambapo Simba ina umri wa miaka 79 tangu ianzishwe imeshindwaje kuwa na jezi za kuuza kwa mashabiki? Kuna majina yanayojiuza mjini hapa kama Mussa Hassan ‘Mgosi’, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu na Hamis Kiiza. Simba imeshindwaje kufanya biashara kwa kutumia migongo ya nyota hao inaowalipa mishahara kila mwisho wa mwezi?
Kessy akomolewa
Ilikuwa ni kituko cha pekee. Beki wa kulia wa timu hiyo, Hassan Kessy aliumia goti wiki iliyopita, hivyo kujiondoa katika programu ya mazoezi ya kawaida ya Kocha Kerr. Baada ya kupata nafuu beki huyo alijuta kuumia. Kocha wa viungo wa timu hiyo, Dusan Momcilovic aliamua kumfanyisha Kessy mazoezi pembeni. Mazoezi aliyofanyishwa Kessy ni mara mbili ya yale waliyofanya nyota wengine klabuni hapo. Kessy alijuta kuumia na siku ya pili alijisalimisha kwa Kerr na kuendelea na mazoezi ya kawaida.
Ivo akasirika kuitwa Matola
Mashabiki wengi wa soka hapa Lushoto wanawafahamu wachezaji na viongozi kwa majina tu na siyo sura jambo ambalo lilimfanya mmoja wa mashabiki hao kumwita kipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda jina la kocha msaidizi Selemani Matola. Mapunda alishangazwa na kitendo hicho kutokana na kuitwa jina la Matola wakati hawafanani kwa sura hata kidogo.
Boda Boda waziba njia
Siku ambayo Simba inawasili mjini hapa waendesha pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda walijitokeza kwenda kuipokea timu hiyo na kuongoza msafara hadi hoteli waliyofikia Simba bila malipo yoyote. Hata hivyo, kitendo cha wachezaji wa timu hiyo kufunga vioo vya basi kiliwakera bodaboda hao ambao waliamua kuziba njia na kuwataka wachezaji wafungue vioo na kuwasabahi. Baada ya kupata salamu kutoka kwa wachezaji, bodaboda hao walilipuka kwa furaha na kurejea katika shughuli zao za kawaida.
Mzee asafiri Km 50 kufuata mazoezi
Mara baada ya kusoma habari kwenye Gazeti la Mwananchi na kuona picha za wachezaji walivyokuwa wamejikunyata baridi, mzee mmoja alilazimika kusafiri umbali wa kilomita 50 kuja kuhakikisha kama hali hiyo ni ya kweli. Mzee huyo alifika katika hoteli ya Simba saa sita mchana na kulazimika kusubiri kushuhudia mazoezi ya jioni ya timu hiyo.