Prisons Hesabu kali mechi ya Yanga

Muktasari:
- Maafande hao wapo katika nafasi ya 13 katika msmamo kwa pointi 30, ambapo Juni 18 wanatarajia kuikaribisha Yanga katika pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapo, kabla ya kumalizia ligi mkoani Singida dhidi ya Singida Black Stars.
TIZI linaloendelea huko Tanzania Prisons kwa ajili ya mechi ijayo dhidi ya Yanga limempagawisha kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah akitamba kuwa kazi ni moja tu kubaki salama Ligi Kuu.
Maafande hao wapo katika nafasi ya 13 katika msmamo kwa pointi 30, ambapo Juni 18 wanatarajia kuikaribisha Yanga katika pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapo, kabla ya kumalizia ligi mkoani Singida dhidi ya Singida Black Stars.
Tangu ligi kusimama, timu hiyo ilitoa mapumziko mafupi ya takribani siku 10, ambapo Juni 2 ilirejea kambini kuendelea na program kwa ajili ya michezo hiyo na kusubiri hatma yake.
Mwanaspoti imeashuhudia mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa yaliyodumu kwa saa nne, huku benchi la ufundi chini ya kocha Josiah akionekana kuwa bize muda wote kutoa maelekezo kwa mastaa wake.
Katika mazoezi hayo, kocha huyo ambaye ni mara ya kwanza kufundisha timu ya Ligi Kuu, alielekeza nguvu katika kumiliki mpira, pasi, kufunga mabao, huku nyota wa timu hiyo wakionyesha morali na hamasa kubwa uwanjani.
Akizungumzia mazoezi hayo, kocha huyo alisema anaridhishwa na utimamu wa wachezaji na kwamba lengo ni kuona analinda heshima yake kubakiza timu Ligi Kuu.
“Vijana wanaonyesha ari na morali, kimsingi naridhishwa na wanachofanya, ninachoomba ni ushirikiano wa wadau na mashabiki ili mechi zilizobaki tunapate ushindi,” alisema Josiah na kuongeza;
“Hakuna mechi rahisi wala nyepesi kwa zilizobaki, tunahitaji mshikamano kufikia malengo, lazima nilinde heshima ya taasisi na mimi binafsi.”