Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ofisa Habari KenGold anusurika kwenda jela

Muktasari:

  • Mkoko alifikishwa mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh1.5 milioni kutoka kwa mchezaji wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital'O ya Burundi.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya Mpira wa Miguu ya KenGold Sport Club, Joseph Mkoko(34), kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miaka miwili baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.

Mkoko anadaiwa kuomba rushwa ya Sh1.5 milioni kutoka kwa mchezaji wa zamani wa  timu ya  mpira wa miguu ya Vital'O ya Burundi, ili amsaidie kusajiliwa na timu yake ya KenGold na kupata upendeleo wa kupangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini hiyo na hivyo kukwepa kifungo cha miaka miwili jela

Hukumu hiyo imetolewa leo, Jumatano Juni 11, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Beda Nyaki,  baada ya mshtakiwa huyo kukiri mashtaka yake.

Mshtakiwa huyo amekiri mashtaka yake leo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kusomewa hoja za awali, ambapo kabla ya kusomewa hoja za awali, alikumbushwa mashtaka yake kwa kusomewa upya na ndipo alipokiri mashtaka yake na mahakama hiyo kumtia hatiani.

Baada ya kutiwa hatiani, hakimu Nyaki alimhukumu.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Nyaki alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri makosa yake na hajaisumbua mahakama, mahakama hiyo inampa adhabu kwa mujibu wa sheria nayo ni kulipa faini ya Sh1 milioni na akikosa atatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,  Wakili wa Serikali Mkuu, kutoka Takukuru, Imani Nitume, alidai upande wa mashtaka hauna kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa huyo.

"Pamoja na kuwa hatuna kumbukumbu za nyuma za makosa ya jinai dhidi ya mshtakiwa huyu, lakini tunaomba mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine," alisema wakili Nitume.

Awali, kabla ya kutolewa uamuzi huo, mshtakiwa alipewa nafasi na Mahakama hiyo ya kujitetea kwanini asipewe adhabu kali.

Mkoko aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa anategemewa na dada na kaka zake na pia bado yeye ana ndoto za kupambana katika upambanaji hivyo anaomba apunguziwe adhabu.

Hakimu Nyaki, baada ya kusikiliza hoja zote, alisema mshitakiwa anamhukumu adhabu ya kwenda jela miaka miwili, au kulipa faini ya Sh1milioni na kwamba haki kukata rufaa ipo wazi iwapo hajaridhika na uamuzi huo.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 13138 ya mwaka 2025 yenye mashtaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa.

Ofisa habari huyo anadaiwa kutenda makosa yake kati ya Disemba Mosi, 2024 hadi Disemba 31, 2024 eneo la Kibaha, mkoani Pwani.

Katika shtaka la kwanza, Mkoko anadaiwa  kuomba rushwa ya Sh1.5milioni  na shtaka pili anadaiwa kupokea kiasi hicho cha rushwa kutoka kwa mchezaji mmoja wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital'o ya Burundi, ili amsaidie kusajiliwa katika timu yake.

Mkoko anadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, iliyofanyiwa  marejeo mwaka 2024.

Kwa mara ya kwanza, Mkoko alifikishwa mahakamani hapo, Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka hayo, hata hivyo alikuwa nje kwa dhamana.