VIDEO: Yacouba nje miezi mitano Yanga

Friday November 19 2021
yacouba pic
By Khatimu Naheka

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yacouba Songne amerejea nchini akitokea Tunisia na sasa uhakika atatakiwa kugusa mpira baada ya miezi mitano kutoka sasa.

Yacouba alirejea jana asubuhi akifuatana na daktari wa viungo wa Yanga, Youssef Mohamed baada ya upasuaji wa goti lake la mguu wa kulia.

Nyota huyo aliumia katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting akicheza kwa dakika 31 kisha kutolewa kwa kujeruhiwa.

Mara baada ya kuwasili Mohamed aliliambia Mwanaspoti, kutokana na upasuaji huo sasa Yacouba atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitano ambapo kuanzia hapo atakuwa tayari ameshaanza mazoezi.

“Lilikuwa ni zoezi lililofanyika kwa mafanikio na kila kitu kilikwenda sawasawa, unajua Profesa Jaleleddine (Dahmane) ni mkongwe katika matibabu haya ya magoti na amekuwa akiwatibu wachezaji wengi wa Afrika Kaskazini,” alisema Mohamed.

Advertisement

“Huu muda wa miezi mitano itahusisha na kuanza mazoezi vizuri, mi ni mgeni hapa Tanzania ila niwapongeze uongozi wa klabu na GSM kufanikisha hili, sio rahisi sana kuona mchezaji anatokea ukanda huu kwenda kutibiwa kule gharama ni kubwa sana.”

Aidha, Mohamed alisema licha ya Yacouba kurejea, lakini atakuwa katika eneo maalum ambalo atakuwa akipewa uangalizi wa karibu ili kuhakikisha anapona na kila hatua ripoti yake itakuwa ikitumwa nchini Tunisia.

“Atakuwa chini ya uangalizi maalum kuhakikisha anapona vyema.”

Advertisement