VIDEO: Ujugu hapaaa… vipi samatta amekunywa chai? Naomba msimpunje sukari

Friday October 02 2020
ujugu pic

UJUGU hapa! ndivyo anavyojulikana zaidi kwenye mtandao ya kijamii, amekuwa akituma ujumbe kibao moja kwa moja kupitia kurasa za wahusika akiwapa ukweli wa mambo katika njia nyepesi kabisa. Alijizoelea umaarufu mkubwa wakati Mbwana Samatta akitua Aston Villa.

Miongoni mwa ujumbe wake ni ile aliyoandika kwenye mtandao wa Aston Villa akiwataka kumpa nafasi ya kucheza Samatta, lakini hakuishia hapo aliendelea kuwataka Villa kumhudumia vyema Samatta ikiwemo kutompunja sukari.

Pia, Aston Villa ilipoachana na nahodha huyo wa Taifa Stars, Ujugu aliendesha kampeni kwa mashabiki kuvunja urafiki na wababe hao wa Jiji la Birmingham na kuelekeza majeshi kwenda Uturuki. Mwanaspoti limemuibukia mafichoni kwenye biashara yake ya kuonyesha mipira maarufu kama kibanda umiza. Lakini, tofauti na zingine hii ya Ujugu ni bonge la Arena kama mwenyewe alivyoipa jina na kubamba.

“Napenda mitandao na ndio maisha yangu, nishakuwa chizi wa mitandao. Naingia kwenye kurasa za watu maarufu na klabu kubwa duniani na kuacha ujumbe ikiwamo ya Donald Trump (Rais wa Marekani), Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Manchester, Arsenal, TFF na nyingine kibao tu,” anaanza kusimulia Ujugu.

Hata hivyo, Ujugu ambaye kama hujapata nafasi ya kukutana naye unaweza kudhani ni mhuni mmoja hivi, lakini jamaa ni mstaarabu mwenye heshima zake. Pia, Ujugu ana familia ikiwemo mke na watoto. Mkewe sio muumini sana na mitandao na hiyo ni changamoto kubwa kwani, kuna wakati wanaingia kwenye mgogoro kwa kuwa, hapendi kumuona Ujugu akitumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, lakini hayo ndiyo maisha yake.

 SMS KWA Trump

Advertisement

Ujugu anafichua kuwa maisha yake ya mtandaoni yalimfikisha hadi kwenye ukurasa wa Trump na kumtuma ujumbe (sms).

“Kuna rafiki yangu anaitwa Dogo Janja alitoa wimbo, nikaingia kwenye page ya Trump nikatuma ujumbe japo hakunijibu, ila nilimwambia: “Trump Dogo Janja ametoa wimbo hapa embu msikilize, nikamtumia na ule wimbo, naamini aliufungua kuusikiliza”.

Anasema mara kwa mara amekuwa akiingia kwenye kurasa za Messi, Ronaldo, Manchester na Arsenal na kufanya yake.

“Manchester siwakubali, hivyo wakifungwa naingia tu kwenye kurasa zao kuwavuruga, lakini huwa wanasoma hata kama hawaelewi kiswahili, japo ninapoandika si lazima nijibiwe,” anasema.

Atoboa siri ya jina la Ujugu

Jina lake halisi ni Nasri Ramadhan lakini Jina la Ujugu lina historia ndefu sana kuanzia shule ya msingi tena darasa la tatu kwenye shule ya Mwembeni, Manyoni, Singida.

Wakati huo baba yake alikuwa akinunua karanga za maganda na kuhifadhi ghalani ili zikipanda bei auze. Lakini, Ujugu kila anapokwenda shule huzama stoo na kuweka mzigo kwenye begi lake kwenda kula na marafiki zake. Yaani bosi yeye.

“Kuna wakati hata daftari nilikuwa nasahau ila shule nakwenda na begi limejaa karanga ndio nikapachikwa jina la Mzee wa Karanga. Lakini, akatokea dogo mmoja na kuanza kuniita ujugu na tangu hapo jina likashika mizizi. Ujugu hapa.

Hata hivyo, anafichua kuwa hakupenda kuitwa hivyo, lakini kadri muda ulivyosonga likawa maarufu kwani, wazazi wake wakaanza kuitwa baba na mama Ujugu.

“Ilikuwa hivyo hivyo hadi sekondari, sikulipenda ila niliona sifa kuitwa mzee wa karanga, lakini kadri nilivyolichukua ndivyo lilizidi kupata umaarufu, majina yangu ya asili yakapotea nikaamua kulizoea na kulikubali hilo jina hadi sasa.

Kumbe ticha wa Msingi

Licha na maneno yake mtandaoni kumtambulisha kama mtu asiyeishiwa visa, Ujugu anasema anachokifanya kwenye mitandao ni kipaji tu ingawa kabla ya kujikita huko alikuwa ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Sikonge Islamic ya mkoani Tabora.

“Mimi ni mwalimu kabisa wa vyeti, baada ya kuhitimu sekondari nilijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kigamboni  Islamic, ambacho kilitujenga kiimani na nilipomaliza nikaanza kazi yangu ya kwanza Sikonge.

“Nilifanya kwa miaka mitatu. Awali, nilipata ajira ya serikali nikapangiwa kwenda Morogoro vijijini huko lakini, sikutaka kwenda huko na kuchagua Sikonge. Nimepewa ajira na cheo hivyo, sikuona sababu ya kuzibia wengine wanaosubiri ajira serikalini,” anafunguka Ujugu.

Hata hivyo, miaka mitatu baadaye Ujugu ambaye alikuwa akifundisha Hisabati na Kiswahili, aliamua kuacha kazi hiyo na kurejea mtaani baada ya mambo kwenda ndivyo sivyo.

 Anauza Kuku

Kutoka kupokea mshahara hadi kurejea uraiani haikuwa kazi rahisi na alilazimika kupambana na maisha.

“Ukiajiriwa kisha ukaingia kwenye biashara mambo huwa magumu sana. Mtaani nilianza kufanya biashara ya kuku nikiwatoa Singida kuja kuwauza Dar, nikafeli. Nikafanya biashara ya vipodozi nako nikachemka na mwisho nikaamua kuanzisha banda la kuangalia mpira. Hapo ikazaliwa Ujugu Arena iliyopo Buza Kanisani, ambayo imeshika mpaka sasa.

“Ujugu Arena haikuwa inabamba sana hivyo, nikawaza nitoke vipi na hapo likaja dili la Samatta kwenye Villa nikaamua kutambaa nayo na wateja wakaongezeka fasta fasta.

 Samatta AMBEBA

Ujugu, ambaye alipata umaarufu kwa jumbe zake kwenye kurasa za Aston Villa kuhusu Samatta, anaeleza kuwa kabla ya Samatta hajatua England, alikuwa akiandika vitu vya kuchekesha mitandaoni.

“Nilikuwa na wafuasi 20,000 ila nilipojikita kwake umaarufu ukaongezeka. Nadili na Samatta kwa sababu namkubali tangu akiwa Mbagara Market, Simba, TP Mazembe na Genk.

“Nilijiuliza, kwanini ashindwe kucheza Aston Villa? Hii timu itaona aibu siku si nyingi, wamemuacha Samatta ambaye alijiunga nayo kipindi ambacho ligi haina msisimko.

“Hawakumpa muda wa kutosha, asingeweza kufanya maajabu wakati walikuwa mkiani wakipambana kushuka daraja. Timu muda wote inazuia Samatta atapata mipira ya kufunga saa ngapi? Hapo bado yule Grealish (Jack) hatoi pasi kwa wakati. Hawa Villa wataona aibu siku sio nyingi kwa Samatta,” anaeleza Ujugu huku akionyesha hisia.

 Neno lake kwa Samatta

Ujugu, ambaye hafichi hisia zake kwa Samatta, anasema hawajawahi kukutana ana kwa ana, japo anaamini kuna siku watakutana tu.

“Sijapata nafasi ya kuonana na Samatta, ila kuna mtu nawasiliana naye ambaye yuko karibu na Samatta na yuko Istanbul, Uturuki hivi sasa amempa jezi aniletee, hivyo Samatta anajua huko nyumbani kuna mtu anaitwa Ujugu,” anaongeza.

Hata hivyo, anasema kuwa siku akikutana na Samatta atamueleza jinsi alivyoufungua milango kwa soka la Tanzania kwenye anga za kimataifa na kuongeza hamasa kwa wachezaji chipukizi kuwa na kiu kama yake.

“Ukimuangalia Samatta hajatokea kwenye akademia, ametokea mtaani tu, amepambana mwenyewe hadi kufanikiwa, huyu mwamba amefungua dunia,” anaeleza Ujugu, ambaye jumbe zake za kwenye mabango yake pale Ujugu Arena zimekuwa zikibamba kinoma.

Kupitia Ujugu Arena na jumbe zake mitandaoni, kwa sasa milango imeanza kufunguka akinasa dili kibao ikiwemo ile ya hivi karibuni kutoka Asas.

 KUMBE NI Arsenal LIA LIA

Licha ya vituko vyake mitandaoni, Ujugu huishiwa pozi kabisa pindi Arsenal inapopewa kichapo huko England na kwenye michuano mingine mikubwa.

“Nililia machozi na sitokaa nisahau, mwaka 2006 Arsenal ilipokosa ubingwa wa Ulaya baada ya kufungwa na Barcelona. Iliniumiza sana na siku hiyo nililia hadharani,” anasimulia Ujugu, ambaye anakiri ni shabiki kindaki ndaki wa The Gunners.

Ujugu kama ulidhani hapa bongo ana mapenzi na mojawapo ya timu kongwe za Simba au Yanga, basi pole yako, jamaa nasema hajawahi kuipenda timu yoyote kati ya hizo.

“Mapenzi yangu kwenye soka la Bongo yapo kwa Mtibwa Sugar, mimi ni mnazi wa timu hiyo, wakati nakuwa naanza kufahamu kuhusu soka mwaka 1999 hadi 2000 Mtibwa anachukua ubingwa wa ligi, nilikuwa niifuatilia timu hiyo na nikajikuta naipenda kutoka moyoni.

“Hata hivi sasa anavyozungumza Haji (Manara msemaji wa Simba) au Nugaz (Antonio wa Yanga), kwenye mitandao, haya maneno maneno yao alikuwa akizungumza Kifaru (Thobias wa Mtibwa), miaka ya 1990. Alikuwa akinivutia sana wakati ule na maneno yake ya kuipamba Mtibwa, sasa hivi kidogo naona umri umekwenda amepunguza makeke yale,” anaeleza.

Anasema kingine kilichokuwa kinamvutia Mtibwa ni namna ilivyokuwa nyumba ya vipaji, hadi timu kubwa za Simba na Yanga zinakwenda kununua wachezaji tena kwa bei mbaya. “Siku hizi tu timu hizo zinaleta wachezaji kwa wingi kutoka nje wengine hawajui hata kutuliza mipira, lakini wazawa wengi wazuri wametoka Mtibwa wakati ule na hata sasa bado wapo.

Kariakoo derby ya Oktoba 18

“Ni mechi nzuri, sijui hata Ujugu Arena kiingilio nitaweka sh ngapi, lakini ni wazi kitaongezeka kidogo. Naamini itakuwa mechi nzuri kushinda hata ile ambayo Yanga iliifunga Simba kwa bao 1-0.

“Simba iko vizuri ina muunganiko na Yanga licha ya kwamba mechi iliyopita walifungwa mabao 4-1, msimu huu wameboresha kikosi chao, wako vizuri zaidi, pamoja na kuwa mechi hii haitabiriki, lakini itakuwa ni nzuri na ngumu kwa kila upande,” anafunguka.

ANGALIZO KWA MORRISON

Usajili wa supastaa kutoka Ghana, Bernard Morrison kutoka Yanga kwenda Simba, umegubikwa na utata mwingi lakini kwa Ujugu hilo hana habari nalo.

Hata hivyo, anadhani kwenye mchezo huo kama Morrison atacheza basi atarajie kukutana na zomeazomea ya kiwango cha kimataifa kutoka kwa mashabiki wa Yanga.

“Morrison sawa mpira anaujua, ametukamata wabongo si Simba na Yanga tu hata TFF, lakini hizi mechi za watani zina presha kubwa. “Hapa inabidi ajiandae kisaikolojia tu, yaani atazomewa sana na ili asitoke mchezoni, japo ni mchezaji mkubwa inabidi kujiandaa kwa lolote tu,” anasema Ujugu.

 

 

 

 

 

Advertisement