VIDEO: Simba yatua Kinshasa matumaini kibao

Muktasari:
Simba imewasili Kinshasa saa 8 mchana tayari kwa mchezo wake wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya wenyeji AS Vita ya DR Congo.
Kinshasa, DR Congo. Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba wamewasili salama jijini Kinshasa, kupokewa na Balozi wa Tanzania nchini DR Congo Luteni Jenerali mstaafu Paul Mella.
Simba imewasili Kinshasa saa 8 mchana tayari kwa mchezo wake wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya wenyeji AS Vita ya DR Congo.
Msafara wa wachezaji wa Simba wamefikia katika hotel ya Venus na saa 11 jioni sawa na saa 1 usiku kwa saa za Tanzania itakwenda kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Martyr ‘Kamanyola’ wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 80,000 utakaotumika kwa mchezo wa Jumamosi jijini Kinshasa.
Akizungumza baada ya kuipokea Simba kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kinshasa, Balozi wa Tanzania nchini Congo Luteni Jenerali mstaafu Paul Mella amewataka wachezaji wa Simba kujituma.
Balozi Mella alisema nimefurahi sana kwa ujio wenu hapa Congo kuiwakilisha Tanzania na sisi tutakuwa pamoja na nyinyi.
“Msiwe na wasiwasi hali ya hapa ni salama, Wakongo wanajua Kiswahili kwa hiyo msishange watu wakiwashingilia,” alisema Balozi Mella.
Mtendaji Mkuu Simba, Crescentius Magori alisema wanashukuru kwa mapokezi waliyopata kutoka kwa Balozi na watanzania.
“Tumekuja Kongo kusaka ushindi hatuja hapa kwa lengo la kujilinda ni matumaini yetu Jumamosi tutapata ushindi,” alisema Magori.
Simba inaongoza Kundi D ikiwa na pointi 3 sawa na Al Ahly zikitofautiana kwa mabao huku, AS Vita na JS Saoura za mwisho.
Simba siyo wageni kwenye Uwanja wa Martyr kwa sababu walicheza uwanjani hapo mwaka 2011, dhidi ya DC Motema Pembe na kufungwa mabao 2-0 hivyo kuondolewa katika mashindano kwa jumla ya mabao 2-1.
Rekodi inaonyesha Simba haijawahi kushinda mechi yoyote katika ardhi ya DR Congo katika mechi zake tatu alizocheza nchini huo amefungwa jumla ya mabao 6-1.
Nchini DR Congo, Simba imefungwa bao 1-0 na AS Vita mwaka 1978, ikachapwa 2-0 na Motema Pembe 2011 kabla ya kunyukwa 3-1 mwaka huo na TP Mazembe jijini Lubumbashi.
Hii ni mara ya tatu kwa Simba na AS Vita kukutana kwenye mashindano ya Afrika.
Timu hizo zilikutana kwa mara kwanza katika hatua 8 bora ya mashindano ya CAF mwaka 1978. Vita ilifanikiwa kushinda kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kuifunga Simba hapa Dar es Salaam 1-0 na marudiano Kinshasa bao 1-0, hivyo historia inaonyesha Simba haijawahi kuifunga Vita katika mashindano yoyote.