Vibonde Shimiwi waanza kupokea vipigo

Muktasari:

Siku moja baada ya pazia la michuano ya Shimiwi mwaka 2021 kutimua vumbi, tayari baadhi ya timu shiriki zimeanza kujiona mwelekeo wake kutokana na kukumbana na vipigo kutoka kwa wapizani wao huku sababu ya vipigo hivyo vikitajwa.

Morogoro. Siku moja baada ya pazia la michuano ya Shimiwi mwaka 2021 kutimua vumbi, tayari baadhi ya timu shiriki zimeanza kujiona mwelekeo wake kutokana na kukumbana na vipigo kutoka kwa wapizani wao huku sababu ya vipigo hivyo vikitajwa.

Akizungumza na Mwanaspoti Online katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, mjumbe wa kamati ya utendaji Shimiwi, Mwajuma Kisengo amesema kuwa michezo hiyo ilisimama tangu mwaka 2018 na baadhi ya timu hazikujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi hali inayowafanya kukumbana na vipigo kwa kukosa ufiti katika michezo mbalimbali ya mashindano hayo.

Mwajuma amesema tayari taswira kwa baadhi ya timu imeanza kujionyesha katika mchezo wa soka na mpira wa kikapu kwa wanawake ‘netiboli’ kwa kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao jambo linaloonyesha kuwa hawakufanya maandalizi ya kutosha kuelekea mashindano ya Shimiwi.

“Kwenye mchezo wa netiboli vipigo vimeanza kwa kasi kubwa na idadi kubwa ya mabao hii inaonyesha timu husika hazikujipanga vyema ndio sababu ya kupoteza huenda michezo inayofuatia hao waliopoteza wakafanya vizuri kwa kubadilika lakini kama wanataka kufanya vizuri michezo ijayo ni lazima wajipange kwa maandalizi.”amesema Mwajuma.

Kocha mchezaji wa timu ya netiboli ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tula Kihaka amesema wamepoteza mchezo dhidi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa vipapu 22-16.

“Hatukufanya maandalizi ya kutosha lakini tunajipanga katika mchezo ujao dhidi ya Ulinzi kwani mchezo huu tuliopoteza kila mchezaji anajua wapi amekosa na nitaenda kurekebisha kasoro zilizojitokeza na kusababisha kupoteza.”amesema Tula.

Kwa upande wa soka timu ya Mahakama Fc ilikumbana na kipigo cha 2-0 mbele ya Kilimo Fc katika mchezo wa ufunguzi wakati Mifugo Fc ikiifunga Hazina Fc bao 1-0.

Katika michezo mingine ya netiboli, Tamisemi imetamba mbele ya Ras Ruvuma kwa kuitandika vikapu 50-5 huku Maliasili ikijipigia Mifugo 27-1 na NFRA ikionja uchungu wa kufungwa kwa kukubali kufungwa vikapu 37-27.

Kwenye michezo ya ufunguzi kwa mchezo wa netiboli, Ukaguzi iliwawabamiza Sanaa kwa kuwachapa vikapu 38-11 huku akinadada wa Ikulu iliwasambaratisha Madini kwa kuwakandamiza vikapu 62-3.