Prime
Utata wa Chama, Simba uko hivi

Muktasari:
- Awali ilidaiwa kwamba staa huyo ameshamalizana na viongozi baada ya kikao cha mtandaoni baina yao. Kocha Abdelhak Benchikha aliulizwa na Mwanaspoti kuhusiana na hatma ya mchezaji huyo
Simba iko Kigoma kukiwasha na Mashujaa na badae itakwenda kwa Tabora United,lakini ishu ya kiungo wao Clatous Chama aliyesimamishwa bado ina utata na hayupo kwenye msafara.
Awali ilidaiwa kwamba staa huyo ameshamalizana na viongozi baada ya kikao cha mtandaoni baina yao. Kocha Abdelhak Benchikha aliulizwa na Mwanaspoti kuhusiana na hatma ya mchezaji huyo lakini akakunja sura na kuonyesha kuhamaki na kusisitiza wachezaji walioondoka ndio watakaotumika kwenye mechi hizo mbili.

“Chama? Bado hajajiunga na timu hawa ndio wachezaji watakaocheza hizi mechi mbili ngumu za ugenini,”alijibu Benchikha kwa kifupi huku akionekana kukunja sura.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema Chama tayari ameshatua nchini lakini bado hajajiunga na timu huku ikielezwa kwamba kuna mazungumzo yanaendelea baina yake na viongozi ingawa Kocha hana taarifa nayo.
Tangu kutua kwa Benchikha, staa huyo hana uhakika kwenye kikosi cha kwanza huku Kocha huyo akionekana kutofurahishwa na ufaza wa baadhi ya wachezaji ambao hauakisi matokeo ya uwanjani.
Aidha Benchikha ameendelea kusisitiza ratiba ya mechi zao hizo ni ngumu ambapo bado hajajua wanakwenda kukutana na aina gani ya viwanja.
“Hizi ni mechi zilizo karibu sana, nimewaambia wachezaji wajiandae sawasawa kiakili, hatujajua tutakwenda kukutana na viwanja vyenye ubora wa aina gani lakini tunatakiwa kwenda kupambana na mazingira yote tutakayokutana nayo huko,”aliongeza.
Wakati huohuo, kikosi cha Mashujaa tayari kipo masikani kwao, Kigoma kikitokea Dar es Salaam kilikokuwa kimeweka kambi maalumu na sasa wanajifua wakiisubiri Simba kwenye mechi ya ligi itakayopigwa Jumamosi, uwanja wa Lake Tanganyika.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Bares’ alisema ratiba ya mchezo huo iliwafikia wakiwa Dar es Salaam na kuamua kusafiri haraka kurejea Kigoma ili kufanya maandalizi ya mwisho kwa utulivu.
“Tulijua mechi hii itapangiwa siku lakini hatukuwaza kama ingekuwa mapema hivi, tulidhani itakuwa kuanzia tarehe sita lakini ndio tayari imepangwa na tumepokea.”
Mchezo huo utakuwa na uhondo wa aina yake kutokana na timu hizo mbili kuwa na maingizo mapya katika vikosi vyao ambapo Mashujaa imewasajili, Samson Madeleke, Eric Johora, Omary Abdallah, David Ulomi, Ibrahim Ame, Reliants Lusajo, Abrahman Mussa, Nyenyezi Juma na Balama Mapinduzi huku Simba ikiwasaini Babacar Sarr, Fredy Michael, Pa Omar Jobe, Ladack Chasambi, Edwin Balua na Salehe Karabaka.
Mashujaa itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa ya pili kutoka mkiani mwa msimamo na alama tisa baada ya mechi 12 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 23 baada ya michezo 10