Joto Zanzibar laitesa Berkane

Muktasari:
- Kwa siku kadhaa tangu kuwasili kwao Zanzibar usiku wa Alhamisi wiki hii, hali ya hewa inayofikia nyuzi joto zaidi ya 32°C mchana imekuwa kero kwa kikosi hicho kutoka Kaskazini mwa Afrika ambako hali ya hewa ni baridi zaidi katika kipindi hiki cha mwaka.
WAKATI kikosi cha RS Berkane kutoka Morocco kikijipanga kuivaa Simba SC katika fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hali ya hewa ya Zanzibar inaonekana kuwatesa Waarabu hao.
Kwa siku kadhaa tangu kuwasili kwao Zanzibar usiku wa Alhamisi wiki hii, hali ya hewa inayofikia nyuzi joto zaidi ya 32°C mchana imekuwa kero kwa kikosi hicho kutoka Kaskazini mwa Afrika ambako hali ya hewa ni baridi zaidi katika kipindi hiki cha mwaka.
Wachezaji wa RS Berkane wamekuwa wakionekana wakilazimika kutumia muda mwingi kunywa maji mara kwa mara hata mazoezini, jambo linaloashiria kutozoea mazingira ya Zanzibar ambayo Simba tayari imeyatumia kama kambi ya maandalizi kwa zaidi ya siku tatu sasa tangu ilipowasili Jumatano wiki hii.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa RS Berkane ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema: “Tunakutana na changamoto ya hali ya hewa. Joto ni kali kuliko tulivyotarajia. Hili linaathiri utimamu wa wachezaji wetu, hasa kwenye mazoezi ya mwisho. Lakini tutapambana hadi mwisho.”

Kwa Simba, hii inaonekana kuwa faida ya wazi, katika mechi ambayo Wekundu wa Msimbazi wanahitaji ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kutwaa ubingwa huo wa CAF, huku mashabiki wa timu hiyo wakiamini hali ya hewa hiyo ni ‘mchezaji wa ziada’ uwanjani.
Je, joto litavuruga mpango wa RS Berkane na kufungua milango ya historia kwa Simba? Jibu litapatikana kesho Jumapili katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kuanzia saa 10:00 jioni baada ya ule wa kwanza Simba kufungwa 2-0 nchini Morocco.
Akizungumzia mchezo huo, kiungo wa RS Berkane, Mamadou Lamine Camara ambaye alifunga bao la kwanza mchezo uliopita, alisema: “Hatujui kama itakuwa rahisi dhidi ya Simba ambayo ni timu nzuri sana. Tupo hapa tukitambua kile kinachotukabili. Tupo kwa ajili ya mechi ya furaha, fainali ni muda wa historia.”
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika wikiendi iliyopita nchini Morocco, mabao ya Camara na Oussama Lamlaoui yaliipa Berkane ushindi wa 2-0.

Hata hivyo, Camara anaamini nafasi walizopoteza katika mechi hiyo ni jambo walilolifanyia kazi ili kuhakikisha hawapotezi ufanisi tena.
“Tulisema hatukufurahishwa sana kwa sababu tulikosa ufanisi. Tulipaswa kushinda zaidi. Lakini muhimu zaidi ni kwamba baada ya mechi ile, tumepata mafunzo mengi. Tumefanyia kazi hilo ili tusirudie makosa katika mechi ya kesho,” alisema.
Camara pia aliweka wazi kuwa kwa sasa hafikirii chochote kuhusu mustakabali wake wa baadaye kwa sababu ana mkataba na RS Berkane na anafurahia maisha ndani ya klabu hiyo.

“Kwa sasa nina mkataba na Berkane. Nina furaha, niko vizuri hapa. Kwa sasa siwezi kuzungumzia siku za baadaye, akili yangu yote ipo kwenye fainali hii ambayo ni muhimu sana kwetu. Baada ya hapo, tutaona,” alibainisha kiungo huyo.