UCHAMBUZI: Utani Simba, Yanga usivuruge akili zetu

Muktasari:
KWA miaka mingi hata kabla ya kupatikana uhuru wa Tanganyika 1961, kila baada ya miezi michache mjadala uliojaa utani wa mchezo kati ya Yanga na Simba ulitanda nchi nzima. Ushindani wa maneno na kupigana vijembe ulishamiri, lakini sura imebadilika siku hizi.
KWA miaka mingi hata kabla ya kupatikana uhuru wa Tanganyika 1961, kila baada ya miezi michache mjadala uliojaa utani wa mchezo kati ya Yanga na Simba ulitanda nchi nzima. Ushindani wa maneno na kupigana vijembe ulishamiri, lakini sura imebadilika siku hizi.
Hapo zamani watani hawa walibadilishana majigambo kwa kuheshimiana na kirafiki, na waliogombana na kukunjana au kutukanana walionekana watu wa ajabu. Nimeona mengi kuanzia katikati ya miaka 1960 hadi katikati ya miaka ya 1980 nilipoandika habari za michezo za timu hizi mbili ambazo zinatambulika kama mahasimu wakuu wa jadi wa soka nchini.
Zamani timu hizi zilikuwa kitu kimoja kabla ya kuchomoza kikundi kilichounda Sunderland ambayo ndio hii leo inaitwa Simba. Siku moja mwaka 1966 nilipofika ofisini Tanganyika Stardard (siku hizi Daily News) katika Barabara ya Maktaba - Dar es Salaam kutoka Magomeni na kuweka Vespa yangu pembeni, niliiona gari la makachero limeegeshwa. Nilidhani ulitokea wizi wa magazeti na makachero walifika kuchunguza.
Polepole nilipanda ngazi kwenda ofisini na kukuta waandishi na wahariri wanadadisiwa na makachero. Nilipomuuliza tarishi, mzee Shaaban kulikuwa na nini, alinijibu: “Hujasoma gazeti”?
Aliniambia habari za Nyerere kufikishwa mahakamani zimeleta kiza zaa. Haraka ninalitafuta gazeti na kukuta habari iliyokuwa na kichwa cha maneno “Nyerere in court” yaani Nyerere Mahakamani. Kichwa hiki cha habari kiliwaudhi wakubwa kwa vile kila aliyeisoma aliamini Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alifikishwa mahakamani.
Ni kweli mtu aitwaye Nyerere alifikishwa mahakamani, lakini alikuwa Hayati Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu. Lakini ili kuuza gazeti kilitafutwa kichwa cha habari cha kuvutia cha kuweka jina la Nyerere.
Mwenendo wa kutafuta vichwa vya habari vya kuvutia bila kujali athari zake unaonekana kushamiri siku hizi. Unanunua gazeti na kukuta kichwa cha maneno cha Waziri kakamatwa ugoni, lakini ukisoma unaona huyo mtu aliyekamatwa ugoni sio mwenye hadhi ya uwaziri, bali jina lake ni Waziri.
Anapotokea kuwepo mtu mwenye jina la Mwinyi au Warioba na kafanya jambo sio la kawaida hutolewa kichwa cha habari cha ajabu. Makachero walipokuwa wanafanya mahojiano niliteremka ngazi na kuondoka na Vespa yangu kwenda Kariakoo.
Huko nilimtembelea mzee aliyekuwa rafiki wa wanamichezo na waandishi wa habari, Hayati Mangara Tabu Mangara, mwenyekiti wa Yanga.
Nilielewana na huyu mzee na hapo nyumbani kwake niliwakuta wachezaji watatu wa Yanga - Abrahman Lukongo, Maulifdi Dilunga na mwingine ambaye nimemsahau. Walikuwa wanaagana na mzee aliyekuwa barazani akiwa amevaa msuli.
Mzee Mangara aliwaambia,”mzaha wenu mnapokutana na Sanda (yaani Sunderland) unatuponza. Hawa sio watu wa kutufunga”.
Nilisalimiana na mzee Mangara na kumpa pole kwa kufungwa na Sunderland siku iliyopita katika mchezo wa kirafiki. Mzee Mangara aliniuliza kama nilikwenda kumsalimia au kumtania. Nilimjibu: “ Yote mawili”.
Alicheka na kuniuliza habari za wazee na marafiki zangu. Mara ikafika gari na kupiga honi mfululizo. Nilipoangalia niliiona Peugeot 304 iliyokuwa maarufu, gari ya mzee Habib, kiongozi wa Sunderland.
Mzee huyu hata Sunderland ilipobadilishwa jina na kuitwa Simba, alisema klabu yake ni Sunderland na sio Simba. Vilevile alijulikana kama Abidjan - jina la utani la Sunderland, lakini mwenyewe alifurahia kuitwa Underline yaani chini ya mstari.
Hii ilitokana na kupenda wachezaji wa pembeni walioukimbiza mpira kwa kasi kuelekea kwenye kibendera cha kona kama hayati Khamis Mtoto na hayati Salim Ali Jinni, na baadaye hayati Willy Mwaijibe wa Simba.
Wakati Sunderland ilipoitwa Abidjan, Yanga ilikuwa pia ikijulikana kama Kuala Lumpur na Kandambili, yaani klabu ya makabwela.
Mzee Mangara alisema: “Haya tena...shetani kafika, laa..haula”. Mzee Habibu aliteremka kwenye gari kwa mbwembwe na mkoba uliokuwa na machungwa, akasalimiana na mzee Mangara na kutaniana, na akamwita mtoto kupokea mkoba wa machungwa.
Mzee Habibu alimtambia mzee Mangara kwa kumwambia,” mtoto wacha kupiga mayowe...waache watu waone wenyewe. Mimi ni mkubwa kwako.”
Mzee Habibu aliongeza: “Wazee wako walijua utapata tabu kwa Sanda na ndio maana unaitwa Tabu Mangara na nataka ujue hutang’ara mbele yangu.”
Akapita muuza kahawa na kashata, na mzee Habibu akanunua birika zima na mkoba wa kashata na kumwambia mzee Mangara hiyo ni zawadi ya Sunderland kwa watoto wao wa Yanga. Mzee Mangara alicheka na kusema: “Ama kweli Mswahili akipata..hulia mbwata.”
Akaitwa mtoto kupokea zawadi ya machungwa ya Habibu, lakini mzee Mangara alionekana kuwa na shaka na ile zawadi.
Mtoto alipopokea mkoba mzee Mangara alimwambia: “Mwambie bibi ampikie chai, maana kwake kafukuzwa na hakunywa chai.”
Wakati huo kila aliyepita barazani alikaribishwa kahawa na kashata. Haukupita muda mrefu mtoto akiwa na mkoba mkono mmoja na mpira wa kuchezea chandimu mkono wa pili na kusema mpira ulikuwemo ndani ya mkoba.
Mzee Mangara alimuangalia rafiki yake na kumwambia:” Nilijua mimi mkoba ulikuwa na mambo yako.” Mzee Habibu alimwambia mtoto, chandimu ni mpira wa babu kwa sababu Yanga walikuwa kama watoto - bora wacheze chandimu.
Mzee Mangara akapokea mpira na kusema: “Ahsante, lakini na wewe unayo siku yako.” Walicheka na kufurahi. Wakaulizana habari za familia, huku wakitaniana. Nilikaa nao kwa muda na kuondoka. Baadaye nilipata habari mzee Habibu alimchukua sahiba wake nyumbani kwa chakula cha mchana.
Niliporudi ofisini nilikuta mhariri wa Sunday News, Thomson (masharubu) amepewa saa 24 kuondoka nchini kwa kubuni kichwa cha habari cha Nyerere mahakamani. Nilipotafakari niliyoyakuta kwa mzee Mangara nilijifunza namna wana wa Yanga na Simba walivyopendana na kutaniana kwa raha na furaha.
Somo nililopata ni namna wazee wa klabu hizi walivyokataa kandanda kuwagawa na kuleta uhasama, bali walilitumia kuimarisha urafiki wa utotoni. Lakini siku hizi mashabiki wakitaniana utasikia wanatukanana au kupigana na hata kukatana visu.
Tujiulize viongozi wangapi wa klabu za sasa wanatembeleana majumbani, kutaniana na kufurahi pamoja? Utani hata katika magazeti umechukua sura ya matusi na kashfa. Viongozi wa sasa wa klabu za kandanda wajiulize kwa nini wenzao licha ya utani uliokuwepo kati yao bado walikuwa marafiki, walitembeleana na kutaniani bila kutukanana wala kupigana.
Nimeirudia simulizi hii baada ya kauli za kashfa na vichwa vya habari vyenye sura mbaya juu ya mchezo wa Yanga na Simba ulioahirishwa karibuni. Lengo langu ni kuwakumbusha wapenzi wa kandanda soka ni burudani na utani sio kutumia lugha chafu.
Ni vizuri viongozi wa klabu wakachukua juhudi za kurejesha maelewano kama ya wazee wale wawili. Hii ianze Yanga na Simba watapokutana katika mchezo ujao wa ligi baada ya ule wa kwanza kuvunjika na kuzua sokomoko lililofika ndani ya Bunge na Serikali kulazimika kutoa tamko la kupoza hali ya hewa.
Imeandikwa na SALIM SAID SALIM