Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TFF, TAKUKURU waanze na kiongozi KenGold

KENGOLD Pict

Muktasari:

  • Ikibainika kuwa ni kweli, waliohusika wapewe adhabu kali na kama itakuwa sio kweli basi mtoa tuhuma aadhibiwe kwa kusema uongo na kuchafua watu.

HIVI karibuni wakati tunasikiliza kipindi cha michezo cha kituo fulani hivi cha redio, kiongozi mmoja wa KenGold ya Mbeya akatoa tuhuma nzito za rushwa kwa baadhi ya maofisa na wachezaji wake.

Akasema kuna timu ya Ligi Kuu iliwahonga baadhi ya wachezaji wake ili wacheze chini ya kiwango na wapinzani wao wapate ushindi kirahisi katika mechi hiyo ambayo ilikuwa muhimu kwa kila upande katika kuhakikisha inapata ushindi ijiweke katika mazingira mazuri ya kukwepa kushuka daraja.

Bila woga wala wasiwasi, kiongozi yule akasema ndiyo maana timu yake iliamua kuwasimamisha baadhi ya wachezaji ambao ndio hapa kijiweni tulisikia wametuhumiwa kuchukua hela ili waihujumu timu yao.

Msimamo wa kijiwe ni kutounga mkono vitendo vyote vya rushwa ambavyo vinalenga kuchochea upangaji wa matokeo kwani athari yake ni kubwa sana kwa mchezo wa mpira wa miguu ambao hapana shaka unaongoza kwa kupendwa na idadi kubwa ya watu Tanzania na duniani.

Hivyo kwa vile hatuungi mkono, tunaomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walifuatilie suala hili na wakibaini lipo, wachukue hatua stahiki ambazo zitakuwa fundisho kwa wale wenye tabia za namna hiyo.

Kama kiongozi wa timu amejitokeza hadharani na kutamka wazi kuwa wachezaji wake wamepata fedha za rushwa, TFF na TAKUKURU wanapaswa kuanza kwa kiongozi huyohuyo kumhoji ili wapate dondoo muhimu ambazo zitafanya wawajue wahusika wake na kuwachukulia hatua.

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kuwa kwenye soka letu kuna baadhi ya watu wamekuwa wakishiriki vitendo vya rushwa lakini hatua huwa hazichukuliwi kwa sababu kunakosekana ushahidi au watu wa kuripoti matendo hayo.

Hivyo wanapojitokeza watu majasiri kama kiongozi huyo wa Kengold, itapendeza kama mamlaka zikamtumia vyema katika harakati za kupambana na jambo hilo kwa vile tayari yeye ana ushahidi na ameusema hadharani.

Ikibainika kuwa ni kweli, waliohusika wapewe adhabu kali na kama itakuwa sio kweli basi mtoa tuhuma aadhibiwe kwa kusema uongo na kuchafua watu.