Tanzania mabingwa Cecafa 2021

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara kwa vijana chini ya umri wa miaka 23, jana jioni iliebeba taji la tatu la mashindano ya Chalenji (CECAFA U-23), baada ya kuifunga Burundi kwa mikwaju ya penalti 5-4, kwenye mchezo wa fainali uliopigwa kwenye uwanja wa Bahir Dar nchini Ethiopia yalipofanyika mashindani hayo.

Mashindano hayo yanayohusisha timu za mataifa wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati kwa sasa yanashirikisha timu za taifa za vijana wasiozidi umri wa miaka 23,  ambao wanachanganywa na wengine watatu waliozidi umri huo kwa lengo la kuongeza nguvu.

Mechi hiyo ya fainali ilikuwa na ugumu kwa timu zote mbili na dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya 0-0 ndipo ikafuata hatua ya kupiga penati na timu zote kufunga penati tano za mwanzo kabla ya Burundi kukosa penati ya sita iliyogonga mwamba wa juu na Tanzania kufunga kupitia kwa Rajabu Athuman na kuwa mabingwa.

Ubingwa huo unakuwa wa tatu kwa Tanzania baada ya kuubeba mwaka 1995 na 2010, walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya fainali dhidi ya Ivory Coast.

Tanzania katika mashindano hayo kwa msimu huu imemaliza bila kupoteza mchezo wowote kwani ilitinga fainali baada ya kuibuka kinara wa kundi A kwa kushinda mechi 1-0 dhidi ya Congo na kutoa sare ya bao 1-1 mbele ya Uganda na kuingia nusu fainali.

Katika nusu fainali, Tanzania ilikutana na Sudan Kusini na kushinda 1-0 kisha kutinga fainali ilipokutana na Burundi walioifika hapo baada ya kuichapa Eriterea bao 3-0 kwenye mchezo wa nusu fainali.