Straika wa Simba aiokoa Zanzibar
Muktasari:
- Heroes ikitumia kikosi cha wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Zanzibar huku ikiwa imewapiga chini mastaa kibao, iliichapa Sudan Kusini mabao 2-1 kwenye mchezo mkali uliochezwa katika Uwanja wa Nyayo.
KIUNGO anayeozea kwenye benchi la Simba, Adeyun Saleh, ameipa Zanzibar Heroes ushindi muhimu kwenye mchezo wa kwanza wa timu hiyo wa Kombe la Chalenji uliochezwa jana Jumatano mchana mjini hapa.
Heroes ikitumia kikosi cha wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Zanzibar huku ikiwa imewapiga chini mastaa kibao, iliichapa Sudan Kusini mabao 2-1 kwenye mchezo mkali uliochezwa katika Uwanja wa Nyayo.
Suleiman Kassim ambaye aling’ara kwenye mchezo huo na kuwapa shida mabeki wa Sudan Kusini, aliifungia Zanzibar bao la kwanza dakika ya saba baada kupiga shuti lililomshinda kipa, Juma Jinaro, na mabeki wa Sudan Kusini ambao walipishana na mpira.
Sudan Kusini ambayo kocha wake ni Mkongomani, Balanga Ismail, ilionekana kupwaya kipindi cha kwanza hasa katika idara ya kiungo, lakini kipindi cha pili ilijipanga na kushangaza ingawa ilishindwa kumzuia Adeyun asifunge dakika ya 67.
Adeyun ambaye aliyesajiliwa na Simba msimu huu, aliingia kuchukua nafasi ya Amour Omary aliyeumia. Bao la kujifuta machozi la Sudan Kusini lilifungwa na Fabian Lako dakika ya 73.
Kocha wa Zanzibar, Salum Bausi, ambaye timu yake ilionekana kuchoka kipindi cha pili alisema: “Ni mchezo ulitubadilikia kwa vile hatukuwa na maandalizi mazuri nikiimaanisha tulikosa mechi za kirafiki, hii timu ni changa sana.
“Nimepukutisha mastaa wengi tegemeo, angalia jinsi Shafih Rajab na Mohamed Faki walivyocheza, wamefanya vizuri sana, nimefurahi, hii ni salamu kwa wengine kwamba tuko vizuri.
“Kuna vitu vichache sana tunakosa kama uzoefu na mechi za kujipima, lakini huu ni ushindi mkubwa kwetu kwa vile haya mashindano ni magumu na tunacheza na timu zilizoko kwenye orodha ya Fifa sisi hatuko.”
Kocha wa Sudan Kusini, Balanga alisema: “Huu ni kama ushindi kwetu kutoka kufungwa mabao 11-0, 6-0 misimu iliyopita mpaka sasa 2-1, ni ushindi. Tuliziambia timu zingine zikae chonjo. Tunakosa uzoefu tu, lakini vijana wangu wana akili.”
Zanzibar itacheza tena keshokutwa Jumamosi mchana na Ethiopia huku Kenya na Sudan Kusini zikicheza jioni siku hiyo.