Stars yapaa wakipewa mchongo

Dar es Salaam. Naibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa , Michezo na Burudani,  AbdallahUlega ameikabidhi bendera timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ huku akiitaka kuzingatia mawili katika michuano ya Chan.
Mambo  hayo ni pamoja na kulinda heshima kwa kuweka mbele utaifa na nafasi ya kila mchezaji kuwa anakwenda kujiuza hivyo wanatakiwa kupambana katika michuano ambayo itawafuatiliwa kwa ukaribu na mataifa mbalimbali.
“Nidhamu, uchezaji mzuri wa uwanjani ndiyo utakaokusaidia kujiuza.Jambo la kwanza ni utaifa na la pili ajira yenu nyinyi namna mtakavyocheza uwanjani,” alisema Ulega ambaye ni mbunge wa Mkuranga.


Taifa Stars imesafiri usiku wa leo kwenda nchini Cameroon kushiriki michuano ya Chan ambayo ni maalumu kwa wachezaji wa ndani.
Katika hafla hiyo, Ulega aliwakabidhi wachezaji hao kitata cha Sh 15 milioni fedha walizoahidiwa kama hamasa ya kueleka mchezo wa kirafiki uliofanyika juzi katika uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
“Pia nimewaletea posho zenu zote za ndani leo (jana), yaani mzigo wote ninao hapa. Tuna imani nanyi msituangushe, ujumbe wetu utakuja siku za mbele,” alisema.
Naibu waziri huyo aliitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuwa na nidhamu katika masuala yote ya kiutawala, akisema asingependa kusikia aibu ya aina yoyote.
“...Ooh mara vijana wanalalamikia hiki mara kile, tunataka TFF mtambue hawa ni mashujaa, simamieni nidhamu. Hakuna longolongo hawa ni watu wazima wanaelewa kila kitu, acheni kufumba fumba linalowezekana linasemwa, kama halijakaa vizuri waambieni ili timu iwe na nidhamu,” alisema Ulega.
Aliitaka TFF kuandaa ripoti ya ushiriki wa Taifa Stars katika mashindano hayo., kuhusu changamoto na namna ya kwenda mbele katika mashindano na michuano mbalimbali.
Akitoa neno la shukrani nahodha wa Stars, John Bocco aliishukuru serikali na TFF kwa namna wanavyojitoa katika timu hiyo, huku akiahidi  kupambana na kuonyesha moyo wa kizalendo katika michuano hiyo na kuwaomba Watanzania kuwaombea.