Stars yafanya kweli ugenini ikiichapa Benin

Muktasari:

TIMU ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imefufua matumaini ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar baada ya kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Benin.

TIMU ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imefufua matumaini ya kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar baada ya kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Benin.

Mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana na dakika ya sita tu Simon Msuva aliipatia bao la kuongoza Stars baada ya kuwatoka walinzi wa Benin na kuingia ndani ya boksi na mpira kisha kupiga shuti kali lilozama moja kwa moja langoni kwa Benin.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Stars ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 huku timu zote mbili zikiwa zimepiga kona mbili kwa kila upande.

Kipindi cha pili kilirejea kwa Stars kuendelea kutafuta bao na dakika ya 51 kidogo Stars ipate bao kwa shambulizi lililotengenezwa kutokea upande wa kulia kwa Israel Mwenda aliyempigia pasi Msuva ndani ya boksi la Benin na kupiga kisigino mpira ukatoka nje kidogo ya goli.

Benin ilifanya mashambulizi ikieendelea kutafuta bao la kusawazisha lakini mipango yake ilikwama kutokana na nidhamu kubwa ya kujilinda kwa wachezaji wa Stars.

Matokeo hayo yanaifanya Stars kufikisha alama saba baada ya kucheza mechi nne na kuongoza kundi J huku ikisikilizia mechi kati ya DR Congo na Madagascar ambapo mechi yaobado haijaanza.

Mechi zilizosalia kwa Stars ni dhidi ya Madagascar ugenini na dhidi ya DR Congo nyumbani na mechi za awali dhidi ya timu hizo, Stars ilishinda 3-2 nyumbani dhidi ya Madagascar na kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya DR Congo ugenini.

Endapo Stars itashinda mechi hizo mbili itaongoza kundi na kuvuka hatua ya makundi kwenda hatua ya mtoano ambapo itacheza na timu mojawapo kutoka makundi mengine nyumbani na ugenini na kama itashinda basi itafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.