Mido ya boli awindwa Azam FC

Muktasari:
- Azam iliyomaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi 63 katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 na kupata tiketi pia ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, imepanga kufanya usajili wake kutokana na kipaji kikubwa alichonacho.
MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, wanaendelea na maboresho ya kikosi hicho kimya kimya kwa ajili ya msimu ujao ili kuleta ushindani, ambapo kwa sasa wameanza mazungumzo ya kuipata saini ya kiungo nyota wa KMC, Ahmed Bakari Pipino.
Azam iliyomaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi 63 katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 na kupata tiketi pia ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, imepanga kufanya usajili wake kutokana na kipaji kikubwa alichonacho.
Taarifa kutoka katika uongozi wa KMC, umeliambia Mwanaspoti Pipino ni miongoni mwa nyota wanaowindwa na timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi, ingawa Azam imeonyesha nia ya kumuhitaji japo hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa rasmi.
“Nafikiri anaweza kuondoka na kwenda kujiunga na Azam kwa sababu yeye mwenyewe pia ameonyesha utayari wa kuchezea huko, kilichobaki kwa sasa ni klabu hizo kukaa zenyewe chini na kukubaliana kuhusu gharama za mauzo,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kilisema hata baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara baina ya timu hiyo dhidi ya Pamba Jiji iliyopigwa Juni 22, 2025 na kuisha kwa sare ya bao 1-1, nyota huyo alimwambia mmoja wa viongozi anahitaji kupata changamoto mpya.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, alisema nyota huyo bado ana mkataba wa miaka miwili zaidi wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho na hakuna ofa iliyowasilishwa mezani kwao kutokea timu inayomuhitaji.
“Tuna ushirikiano mzuri sana na Azam na kama ni kweli wanamuhitaji wangeleta barua rasmi, ila hadi sasa tunapozungumza hakuna suala hilo, tunachohitaji ni kuona taratibu na misingi iliyowekwa inafuatwa na sio vinginevyo,” alisema Daniel.
Pipino aliyejiunga na KMC katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea kituo cha Akademia cha Magnet, ameonyesha kipaji kikubwa na kuanza kuzivutia timu mbalimbali kwa ajili ya kuinasa saini yake, huku Azam ikiwa ni miongoni mwao pia.
Nyota huyo alianza kung’ara akiwa na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 (U-20) ya Ngorongoro Heroes, iliyotwaa ubingwa wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), baada ya kuifunga Kenya mabao 2-1 katika fainali.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam Oktoba 20, 2024, iliipa nafasi Ngorongoro ya kushiriki fainali za AFCON (U-20), zilizofanyika Misri mwaka 2025, na kuishia hatua ya makundi.